KILA Mtanzania katika miezi miwili ijayo, atakuwa analala ndani ya chandarua katika jitihada za Serikali kupambana na malaria inayoendelea kuua watu wengi nchini.
Habari hizo zilitangazwa usiku wa kuamkia jana na Rais Jakaya Kikwete alipohutubia Mkutano wa 12 wa Wadau na Watafiti wa Dawa za Malaria (MMV).

 
Mkutano huo wa siku mbili wa mabingwa wa kupambana na malaria kutoka mataifa mbalimbali unafanyika Dar es Salaam. Rais Kikwete alisema malaria inabakia, kama ambavyo imekuwa kwa muda mrefu kuwa tishio kubwa kwa afya, ustawi, uzalishaji na maendeleo ya Watanzania na Waafrika kwa jumla.

Aliongeza kuwa Serikali yake imedhamiria kutokomeza ugonjwa huo, kwa kutumia njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kugawa bure vyandarua vya kukinga wananchi dhidi ya mbu wanaosababisha ugonjwa huo.


Alisema malaria si matokeo ya umasikini wa Waafrika, bali ni chanzo na sababu kuu ya umasikini ambapo ugonjwa huo unagharimu uchumi wa Afrika dola bilioni 12 za Marekani kwa mwaka, kwa kuhudumia wagonjwa na asilimia 1.3 ya mapato ya mataifa hayo kupotea.


“Malaria pia ni mchangiaji na chanzo kikuu cha vifo vya akinamama na watoto katika Afrika na hivyo kuwa kikwazo kikubwa katika kuchelewesha ufikiwaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG),” alisema.


Hata hivyo, Rais Kikwete alielezea mafanikio makubwa ambayo yamepatikana katika kupambana na malaria Afrika.


Alisema: “Katika miaka mitano iliyopita, matumizi ya vyandarua, unyunyiziaji wa dawa na matumizi ya dawa zinazofanya kazi vizuri umepunguza malaria kwa asilimia 50 katika nchi 11 za Afrika.


“Sasa malaria imepoteza nafasi yake kama mwuaji wa kwanza wa watoto wadogo wenye umri wa miaka mitano na kushikilia nafasi ya tatu,” alisema Akikariri takwimu za Ripoti ya Malaria ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa mwaka jana, Rais Kikwete alisema kiasi cha vyandarua milioni 289 vimegawanywa Afrika kati ya mwaka 2008 na 2010, idadi inayotosha kukinga asilimia 76 ya wakazi wa Bara hilo wanaokabiliwa na hatari ya kupata malaria.


“Idadi hii ni kubwa sana kwa kutilia maanani kuwa mwaka 2000 idadi hiyo ilikuwa ni asilimia tano tu,” alisema.


Kuhusu unyunyiziaji wa dawa, Rais alisema mwaka 2009 watu milioni 73 katika nchi za Afrika waliepukana na malaria kutokana na dawa hiyo, ikilinganishwa na milioni 13 mwaka 2005 na dawa mseto milioni 229 zilinunuliwa duniani mwaka 2009 ikilinganishwa na milioni 2.1 mwaka 2003.


Akizungumza katika shughuli hiyo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda, alisema watu kati ya 60,000 na 80,000 hupoteza maisha kila mwaka kwa malaria.


Kwenye shughuli hiyo, Rais Kikwete pia alishuhudia aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya MMV kwa miaka sita iliyopita, Baroness Lynda Chalker wa Uingereza, akikabidhi uenyekiti kwa Raymond Chambers wa Marekani ambaye pia ni Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa UN katika kupambana na malaria.