SERIKALI imepanga kuwaondoa kwa nguvu wavamizi wa ardhi ya Kambi ya Jeshi la Wananchi ya KTC Kunduchi, Dar es Salaam wakiwemo wachimba kokoto.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Meck Sadiki alisema wachimbaji kokoto wamekuwa wakifanya uchimbaji kwa kulipua baruti, jambo ambalo linaweza kusababisha milipuko ya silaha zilizohifadhiwa ndani ya Kambi ya Jeshi.
Akizungumza na waandishi wa habari juu ya tatizo la uvamizi huo wa ardhi katika Jiji la Dar es Saam, Sadiki alisema Wilaya ya Kinondoni inaongoza kwa kuwa na wavamizi wengi. Zaidi ya hekari 250 zinamilikiwa na watu 9 kinyume na utaratibu.
Alisema, wananchi hao wamethubutu kuvamia hadi eneo la Kambi ya Jeshi, na kwamba mbali ya meta 500 waliyotakiwa kuishi kutoka usawa wa kambi, wamevamia na kukaribia hadi meta 50.
Sadiki alisema, uwepo wa kambi hiyo katika eneo lile, si kwa bahati mbaya bali iliwekwa kwa sababu maalumu hivyo wananchi wanapaswa kuheshimu wanachoelezwa kuhusu eneo hilo.
“Wapo waliojenga nyumba na vibanda vyao karibu kabisa na maeneo ya kambi, lakini pia wapo wanaoendelea kuchimba kokoto kuelekea eneo hilo, hawa wote tumewalea kwa kipindi kirefu kilichobaki ni kuchukua hatua kali dhidi yao” alisema Sadiki.
Aidha Sadiki amewataka watu wote wanaomiliki ardhi kihalali ndani ya maeneo mbalimbali ya Jiji, kuyaendeleza kwa ujenzi ili kuepusha uvamizi toka kwa watu wasio waaminifu.
0 Comments