Jeshi la Sudan limefanya mashambulizi ya anga ikiwa ni kampeni ya kijeshi katika jimbo la Kordofan Kusini.
Eneo hilo lina mzozo unaoingia siku ya kumi sasa na kusababisha maelfu kukimbia.
Inaripotiwa kuwa mapigano yamekuwa makali kati ya vikosi vya serikali na wanajeshi wa zamani wa jeshi la Kusini.

Sudan Kusini imebakisha siku kadhaa kabla nchi hiyo kubwa barani Afrika haijagawanywa.
Mwandishi wa BBC Peter Martell aliyeko mji mkuu Juba anasema ndege za jeshi la Sudan Kaskazini zimelipua eneo la kijeshi la anga lililoko Kauda katikati ya milima ya Nuba, kwenye makazi ya makundi yanayounga Sudan Kusini likiwaita waasi.
Umoja wa mataifa unaripoti kuwa milio mikubwa ya risasi iliweza kusikika huku mapigano yakisambaa katika jimbo la Kordonfan Kusini.
Zaidi ya watu 53 elfu wanakadiriwa kuyakimbia mapigano hayo.
Wafanyakazi wa mashirika ya misaada wanasema wamezuiliwa kufaya kazi yao huku maeneo muhimu yakiwa yamefungwa, na kusababisha mateso kwa raia.
Ndege za misaada zimezuiliwa kutua kwa wiki nzima sasa huku wanapiganaji wenye silaha wakiwa wameweka vizuizi barabarani.
Kuna wasiwasi kuwa idadi ya watu waliokufa ikaongezeka, huku wafanyakazi wa misaada na viongozi wa dini katika eneo hilo wakisema kuwa wanaolengwa ni wale wanaoaminika kuipinga serikali ya Khartoum.
Watu wanachimba mahandaki wakiogopa mashambulizi zaidi.
Awali wafanyakazi wa misaada walisema mapigano yanazidi kuongezeka katika jimbo la Nuba, ambako ni makazi ya makabila ya waafrika ambao wana uhusiano zaidi na Sudan Kusini kuliko Kaskazini inayokaliwa na waarabu wengi.