Rais Jakaya Kikwete, amewaagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kutopokea barabara zitakazojengwa  chini ya viwango vya ubora na wakandarasi.
Vile vile, amewajia juu watumishi wa mizani nchini kuwa wanachangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa barabara kwa kuendekeza vitendo vya ulaji rushwa kwa magari yanayozidisha uzito.

Rais aliyasema hayo jana wakati akifungua barabara ya Usagara hadi Geita yenye umbali wa kilometa 90 na iliyoigharimu Serikali ya Tanzania Sh. bilioni 78.7.
Alisema barabara hiyo imejengwa kwa pesa za serikali bila kutegemea hata senti moja ya wafadhili na akasisitiza kuwa bado serikali inahitaji misaada ya wafadhili katika shughuli zake mbalimbali.
“Barabara nyingi zinajengwa na kukabidhiwa lakini muda mfupi baadae zinaharibika, hivi wakati wote wa ujenzi mkandarasi msimamizi anakuwa wapi,” alihoji.
“Utakuta mkandarasi msimamizi anakataa kuipokea barabara baada ya kukamilika akidai kuwa haijajengwa katika viwango vya ubora, alikuwa wapi wakati wote, kama inajengwa chini ya viwango kwanini asimzuie kuendelea kujenga kama alikuwa anamsimamia,” alisema.
 Rais Kikwete alisema kitendo cha baadhi ya wafanyakazi wa Tanroads kupokea rushwa na kuruhusu magari yenye uzito mkubwa kupita katika barabara inaleta picha mbaya kwa wageni kwani wapo wanaoombwa rushwa baada ya kupitisha magari yenye uzito mkubwa.
Pia, aliwataka wakala hao wa barabara kuzikagua mara kwa mara barabara ili kujua kama zimeanza kuharibika na kuzifanyia marekebisho haraka kabla hazijaharibika zaidi.
  “Unaweza kukuta barabara imeanza kuwa na kishimo kidogo, lakini meneja wa Tanroads anapita hapo hapo, Mkuu wa Wilaya naye anapita hapo hapo na hata Rais naye anapita hapo hapo, lakini shimo hilo litaachwa hadi liwe kubwa, kwanini lisizibwe mapema,?” alihoji Kikwete.
Naye Waziri wa Ujenzi, John Magufuli alisema kuanzia sasa mkandarasi atakayekamilishja ujenzi wa barabara na kuikabidhi, ataendelea kuwepo katika eneo la mradi kwa kipindi cha miaka mitatu tangu mradi huo ulipokamilika.
 Alisema awali mkandarasi alikuwa akikaa mwaka mmoja, lakini sasa atakaa kwa miaka mitatu na iwapo barabara itaharibika katika kipindi hicho, atakuwa akiitengeneza kwa gharama zake.
Pia, alisema wakandarasi 7,000 waliosajiliwa nchini, kati yao 2,009 wamefutiwa usajili kwa kushindwa kutekeleza miradi wanayopewa.
 Alisema wataendelea kusimamia barabara kwa sheria zilizopo ili zisiharibike na hawatawaonea huruma kuwatimua makandarasi watakaoshindwa kutekeleza kwa wakati miradi waliyopewa.
  Barabara hiyo imejengwa na Kampuni ya Sinohydro ya China.
CHANZO: NIPASHE