Serikali imezitaka taasisi za sekta binafsi nchini kuwekeza katika nishati kwa lengo la kusaidia upatikanaji wa umeme.
Wito huo ulitolewa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu(Pichani juu), alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa 12 wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania.

Alisema taasisi hizo zinatakiwa kujikita katika kutafuta suluhisho la upatikanaji wa nishati ya umeme badala ya kuiachia serikali peke yake.
"Tatizo la umeme halipo kwa serikali peke yao hivyo taasisi binafsi nazo zinatakiwa kuwekeza katika nishati ya umeme ili kuondoa malumbanano yanayojitokeza," alisema Dk. Nagu
Alisema endapo watazingatia jambo hilo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza tija ya viwanda na kuvipa nafasi ya ushindani katika masoko ya nje.
Aidha, alisema serikali inatambua umuhimu wa kuendeleza rasilimali watu pamoja na masuala ya ujuzi ikiwa na lengo la kutekeleza shughuli zote za uchumi kwa ufasaha.
Alisema suala hilo limekuwa ni changamoto kubwa kwa wajasiriamali wengi ambao wanakosa ujuzi wa msingi katika kuhakikisha biashara zao zinakuwa endelevu.
Dk. Nagu alisema serikali inatambua mchango mkubwa unaofanywa na taasisi za sekta binafsi na kuahidi kushirikiana nazo.
Alisema pamoja na mafanikio yaliyofanywa na taasisi hizo katika kutekeleza miradi yake kwa lengo la kuwanyanyua kiuchumi wajasiriamali, jambo la muhimu ni kuongeza juhudi kuhakikisha zinawafikia walengwa wengi katika Soko la pamoja la Afrika Mashariki.
Dk. Nagu amezitaka sekta binafsi kuhakikisha zinakuwa na ushirikiano na sauti moja bila kuwepo kwa makundi ili watekeleze majukumu yao katika kukuza uchumi wa taifa.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini, Esther Mkwizu, aliishukurui serikali kwa msaada mkubwa wanaopata katika kufanikisha kutekekeza majukumu yao.
Alisema suala la kuwekeza katika nishati ya umeme watalifanyia kazi kwani kumekuwa na ongezeko kubwa ya mahitaji ya nishati hiyo.(Source-Nipashe)