Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akichangia hotuba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, bungeni mjini Dodoma.(Picha na Maelezo).

WAZIRI Mkuu mstaafu, Edward Lowassa amesimama kwa mara ya kwanza bungeni tangu alipojiuzulu wadhifa huo kwa kashfa ya Richmond, na kuishangaa Serikali kwa kuogopa kufanya maamuzi.

Akichangia katika hotuba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliyoitoa bungeni juzi, Lowassa alisema viongozi wa Serikali wameingiwa na ugonjwa wa kuogopa kutoa maamuzi kwa mambo mbalimbali hatua inayokwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.



“Hivi sasa mmeingiwa na ugonjwa mbaya wa kuogopa kufanya maamuzi, acheni mara moja mtindo huo, fanyeni uamuzi. Ni heri ukalaumiwa kwa kufanya uamuzi mbaya kuliko kutofanya uamuzi kabisa,” alisema Lowassa aliyeshangiliwa sana na wabunge.


Alisema Serikali ya CCM imefanya mambo mengi katika miaka 50 ya Uhuru wa Taifa, lakini akasema hatua hiyo inatokana na hatua ya viongozi waliotangulia Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa kuthubutu.


Alisema kama Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete itathubutu na kuweza kujenga reli ya kati, itaboresha bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga uchumi wa Taifa utaimarika zaidi.


Alisema inashangaza kuona kuwa wapo watu wanaobeza maendeleo yaliyofanywa na Serikali ya CCM katika kipindi cha miaka 50 ya Uhuru na kusema kuwa watu hao hawajui historia ya Taifa la Tanzania.


“CCM imejenga barabara za lami, CCM imejenga mradi wa maji wa Ziwa Victoria, CCM imejenga sekondari za Kata na CCM imejenga Chuo Kikuu kikubwa zaidi katika nchi za Afrika Mashariki na Kati cha UDOM (Chuo Kikuu cha Dodoma), haya ni maendeleo makubwa,” alisema Lowassa.


Akitumia msemo “Dunia inajua na Watanzania wanajua”, Lowassa alisema maendeleo hayo si ya kubeza lakini alisema Serikali isiogope kuendelea kuchukua hatua za kutekeleza miradi ya maendeleo.


“Tusiogope, tunaweza kujenga reli ya kati, tusiogope tunaweza kuboresha miundombinu ya Bandari ya Mtwara, Bandari ya Tanga, Bandari ya Dar es Salaam. Najua mtasema fedha tutapata wapi… fedha zipo.


“Tumeweza kujenga UDOM kwa fedha zetu za ndani zaidi ya trilioni moja. Tunaweza kujenga reli. Tunaweza kutumia utajiri wa gesi yetu asili ya Mtwara kukopa fedha na kujenga miradi hii, tusiogope,” alisema Lowassa.


Alisema hakuna sababu ya Tanzania kuogopa kukopa kwa kisingizo cha kuogopa kuongeza deni la Taifa na kwamba hata nchi kama Marekani hivi karibuni ilikopa fedha kwa ajili ya maendeleo bila kuogopa kuongezeka kwa deni la Taifa.


Alisema hatua ya ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa asilimia 7 si ya kubeza kwani inadhihirisha namna Serikali inavyokuza uchumi wake, lakini alionya kuwa ni lazima ukuaji huo wa uchumi uweze kutafsiriwa katika maisha ya wananchi wa vijijini.


Katika hatua nyingine aliishauri Serikali kuiondoa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwa vile inaonesha kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imeelemewa na kazi na hivyo kuchelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.


Aliitaka Serikali kuchukua hatua ya kushughulikia tatizo la maji katika Jimbo la Monduli na pia kushughulikia tatizo la njaa katika jimbo hilo linalotokana na ukosefu wa mvua kwa misimu miwili sasa.


Aliishukuru Serikali kwa kuwapa chakula cha msaada wananchi waliokumbwa na tatizo hilo la njaa msimu uliopita.


  .