KAMANDA wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Adolfina Chialo(Pichani), amewataka wananchi na madereva kuwafichua askari wanaowaomba rushwa kabla ya kuwafanyia usaili kwa ajili ya kuwapatia leseni mpya.
Chialo, alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Morogro baada ya Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Fatma Mwassa, kufungua mkutano ulioandaliwa na Chama cha Madereva wa Mabasi Tanzania na Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji nchini kwa madereva wa Morogoro kuhusu utaratibu wa utoaji wa leseni mpya za magari.
Kamanda alisema wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi.
Alisema, milango ipo wazi kwa mtu yeyote kuwasilisha taarifa sahihi kwa maofisa wa juu wenye dhamana ili hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya askari atakayebainika kwenda kinyume na maadili.
“Vitendo vyovyote vya kuombwa kutoa rushwa kwa askari wetu vitolewe taarifa na hili ni pamoja na madereva wanaohitaji kupata leseni mpya , tupeni taarifa za askari hao ili hatua za kinidhamu zichukukiwe dhidi yao ” alisema Kamanda huyo.
Awali, Katibu Mkuu wa Chama cha Madereva wa Mabasi Tanzania , Salum Abdallah alisema kumeibuka tatizo la uchakachuaji wa vyeti vya udereva kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya vyuo vya fani hiyo visivyotambuliwa kisheria. “
Vyeti hivi vinachakachuliwa mitaani kwenye vyuo hivyo na watu wasiowaaminifu …Chama chetu hakitakuwa tayari kupakwa matope na madereva wa aina hii na tunaahidi tunawachukulia hatua zinazostahili,” alisema Abdallah.
0 Comments