SERIKALI imeahidi kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi wa umma wake, huku ikitangaza juhudi za kudhibiti matumizi yake kwa kusitisha ununuzi wa magari, kupunguza posho mbalimbali na ununuzi wa samani za ofisi hususan zile zinazoagizwa nje ya nchi. 
Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo alisema hayo jana wakati akiwasilisha bungeni mjini Dodoma Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2011/2012. 
Kuhusu maslahi ya watumishi, Mkulo alisema Serikali itaendelea kuboresha maslahi hayo
kulingana na uwezo wa mapato yake kwa lengo la kuwawezesha kumudu gharama za maisha.

Lakini Waziri Mkulo alisema Waziri mwenye dhamana ya Utumishi, atatoa maelezo zaidi kuhusu suala hilo wakati atakapowasilisha makadirio ya Wizara yake.


“Maeneo ambayo yatatiliwa mkazo ni pamoja na malipo ya mshahara na likizo kwa wakati, kuhakikisha watumishi wanalipwa mafao yao mara baada ya kustaafu, pamoja na pensheni zao za kila mwezi.


“Sambamba na hayo, Serikali itatoa mafunzo kwa maofisa wa Hazina ndogo wa Mahakama zote zinazoshughulikia mirathi, na kuweka mikakati ya pamoja kuwaondolea kero wasimamizi na warithi wa mali ya marehemu,” alieleza Waziri Mkulo.


Katika kudhibiti matumizi yake, Mkulo alisema Serikali katika mwaka wa fedha 2011/12, itasitisha ununuzi wa magari ya aina zote isipokuwa kwa sababu maalumu na kwa kibali cha Ofisi ya Waziri Mkuu.


Vile vile, Serikali itasitisha ununuzi wa samani za ofisi hususan zile zinazoagizwa nje ya nchi; kupunguza malipo ya posho mbalimbali yasiyokuwa na tija; kupunguza matumizi ya mafuta kwa magari ya Serikali na kupunguza safari za ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na ukubwa wa misafara.


“Na pia kuendelea kupunguza uendeshaji wa semina na warsha isipokuwa pale inapobidi na kwa kibali cha Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na kupunguza gharama za maonesho na sherehe mbalimbali,” alifafanua Mkulo juhudi hizo za kudhibiti matumizi ya Serikali.


Katika kudhibiti matumizi, Mkulo alifafanua zaidi kuwa Serikali imepanga kufanya sensa ya watumishi wote wa Serikali na taasisi zake kwa kuandaa siku maalumu ya malipo ya mshahara dirishani.


Alisema Serikali itasimamia utekelezaji wa Waraka Namba 2 wa Hazina wa mwaka 2010 kuhusu uwajibikaji na udhibiti katika usimamizi wa malipo ya mishahara pamoja

na ukamilishaji wa maboresho ya mfumo wa kuandaa mishahara utakaoimarisha udhibiti
wa malipo ya mshahara.

Mkulo alisema Bajeti hiyo ya Serikali itazingatia vipaumbele vya umeme, maji, miundombinu ya usafiri na usafirishaji (reli, bandari, barabara, viwanja vya ndege

na Mkongo wa Taifa), kilimo na umwagiliaji na kupanua ajira kwa sekta binafsi na ya
umma.

Akizungumzia maeneo ya kipaumbele katika mchanganuo wa bajeti, alisema miundombinu

ya barabara, reli, bandari na Mkongo wa Taifa zimetengewa Sh trilioni 2.78 ikilinganishwa na Sh trilioni 1.5 mwaka 2010/11 sawa na ongezeko la asilimia 85.

Mkulo alisema kipaumbele cha pili ni elimu iliyotengewa Sh trilioni 2.28 ikilinganishwa na Sh trilioni 2.04 mwaka 2010/2011, sawa na ongezeko la asilimia 12.


Afya imetengewa Sh trilioni 1.209 ikilinganishwa na Sh trilioni 1.205 kwa mwaka 2010/11, sawa na ongezeko la asilimia 0.3 na kilimo na umwagiliaji kimetengewa Sh bilioni 926.2 ikilinganishwa na Sh bilioni 903.8 mwaka 2010/2011 sawa na ongezeko la asilimia 2.5.


Kipaumbele cha tano ni maji na kimetengewa Sh bilioni 621.6 ikilinganishwa na Sh bilioni 397.6 mwaka 2010/11 sawa na ongezeko la asilimia 56.


Nishati na Madini inakamilisha kipaumbele cha sita kwa kutengewa fedha nyingi ikiwa imetengewa Sh bilioni 539.3 ikilinganishwa na Sh. bilioni 327.2 mwaka 2010 sawa na ongezeko la asilimia 65.


Aidha, Mkulo alieleza kuwa Serikali imefanya mabadiliko katika muundo wa Wizara ya Fedha kwa kuifanya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa wakala anayejitegemea, kwa lengo la kuzisimamia kwa karibu, wakala, taasisi na mashirika ya umma na hivyo kuongeza ufanisi, tija, mapato na kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka Serikali Kuu.


Mkulo akizungumzia ongezeko la bei ya mafuta ya petroli, alisema Serikali imeamua kufanya mapitio ya kukokotoa tozo zinazotozwa na mamlaka mbalimbali kwa lengo la kuzipunguza na zoezi hili litakamilika katika mwaka wa fedha 2011/2012.


Alisema Serikali pia inakamilisha utaratibu wa ununuzi wa mafuta kwa wingi kwa lengo la kuziuzia kampuni za usambazaji kwa bei ya jumla.


Alisema kanuni zitakazotoa mwongozo katika uagizaji wa mafuta kwa pamoja, zimekamilika na utaratibu huu unategemewa kuanza katika mwaka huu wa fedha wa 2011/2012.


Alisema nia ni kupunguza bei na gharama za usafirishaji wa mafuta hayo. Kwa kutambua umuhimu wa vitambulisho vya Taifa, Serikali imekamilisha taratibu za kumpata mzabuni na tayari mkataba umekwishasainiwa.


Mkulo alisema mradi huo utagharimu Sh bilioni 355 mpaka utakapokamilika; na kwamba kwa mwaka 2011/12, Sh bilioni 70 zitatumika kama ilivyopangwa.


“Awamu ya kwanza ya uzalishaji wa vitambulisho hivyo itakamilika mwishoni mwa 2011,” alisema Mkulo na kuongeza: “Mradi huu ukikamilika utawezesha wananchi kuwa na vitambulisho na hivyo kusaidia, pamoja na mambo mengine, kuongeza wigo wa ulipaji kodi, kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na huduma za kifedha na

kuwatambua maharamia haramu.”

Mkulo alisema Serikali itatekeleza majukumu mengi ikiwamo kulipa kiasi cha Sh bilioni 10.5 kwa ajili ya madeni ya watumishi wa Serikali za Mitaa wasio walimu kulingana na uhakiki uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.


Mengine ni ujenzi wa hospitali tatu za mikoa ya Manyara, Singida na Mbeya pamoja na ukarabati wa hospitali 10 za mikoa na 17 za wilaya; ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma, nyumba tatu za wakuu wa mikoa, ofisi 22 za halmashauri na nyumba 210 katika halmashauri.