WAFANYAKAZI watatu wa Mahakama ya Mwanzo Ukonga akiwemo Hakimu wa Mahakama hiyo, Ndevera Kihenga wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya kuomba na kupokea rushwa ya Sh 100,000.
Washitakiwa wengine walisomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Rita Tarimo ni Karani wa Mahakama, Evelyn Mowo na Mhasibu Victoria Mtasiwa.
Wakili wa Serikali, Salha Abdallah alidai mahakamani hapo kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matatu likiwemo la kupokea rushwa ili watoe dhamana kwa mshitakiwa.
Ilidaiwa kuwa Aprili 24 mwaka huu katika Mahakama ya Mwanzo Ukonga, washitakiwa Kihenga na Evelyn walidaiwa kuomba rushwa ya Sh 100,000 kutoka kwa Joyce Msaki kwa lengo la kumpa dhamana.
Abdallah alidai kuwa Joyce aliyekuwa na kesi mbele ya Hakimu Ndevara alitakiwa kutoa fedha hizo ili apewe dhamana.
Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa Mei 24 mwaka huu katika mahakama hiyo, Hakimu Ndevera alipokea rushwa ya Sh 40,000 kutoka kwa Joyce kwa lengo la kumpa dhamana.
Abdallah alidai katika shitaka la tatu kuwa, Mei 27 mwaka huu washitakiwa wote kwa pamoja walipokea Sh 60,000 kutoka kwa Joyce kwa lengo la kumpa dhamana.
Washitakiwa walikana mashitaka na kuachiwa kwa dhamana hadi Juni 22 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena, na upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika .
0 Comments