TANZANIA WHITE HOUSE.

Kwa mara nyingine, wabunge wamehoji mwenendo wa serikali wa kukarabati Ikulu ya Rais ya jijini Dar es Salaam kila mwaka kwa kutumia mabilioni ya shilingi, badala ya fedha hizo kutumika kwa shughuli nyingine za maendeleo nchini.
 Safari hii hoja hiyo iliibuliwa upya na Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Susan Lyimo, alipokuwa akichangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012, bungeni, mjini hapa jana.

 Lyimo, alisema kwa mfano tangu mwaka 2001 mpaka leo, ukarabati wa Ikulu ya jijini Dar es Salaam, umegharimu Sh. bilioni 56.
 Alisema kila mwaka, kuanzia mwaka huo, kumekuwa na ukarabati wa Ikulu, ambao umekuwa ukitengewa zaidi ya Sh. bilioni 2.
 Lyimo alisema mwaka jana ilitengewa Sh. bilioni 7.2 na mwaka huu, wameomba bilioni 10 kwa ajili ya ukarabati Ikulu ya Rais. 
“Lazima tujiulize. Hivi kweli ni nyumba gani, ambayo inakarabatiwa kila mwaka? Yaani kila mwaka, kuanzia mwaka 2001, 2002, 2003 mpaka leo hii Ikulu ya Rais inaendelea kukarabatiwa na kwa fedha nyingi,” alisema na kuongeza: 
“Hivi fedha hizi zisingeweza kutosha kukarabati au kuendeleza Ikulu iliyoko Chamwino ili Rais aweze kuhamia Dodoma? Mimi naamini kabisa Rais akihamia Dodoma, hakuna waziri atakayebaki Dar es Salaam.”
 Alisema kuna mbunge aliyewahi kupendekeza Spika wa Bunge ahamie Dodoma na kusema hata kama Spika akihamia Dodoma, kama Rais hayuko Dodoma haitakuwa na athari kwa sababu Rais na Waziri Mkuu ndio watendaji wakuu wa serikali. 
“Lakini ukiangalia bado Waziri Mkuu anaomba aidhinishiwe fedha kwa ajili ya makazi ya Dodoma na ofisi Dar es Salaam,” alisema Lyimo.
 Lyimo alisema pia tangu katika Bunge la Tisa wamekuwa wakipigia kelele ndani ya Bunge suala la ukubwa wa Baraza la Mawaziri, lakini mpaka leo bado ni kubwa sana lenye mawaziri 54 ikijumuisha na rais, makamu wake pamoja na Waziri Mkuu na Rais wa Zanzibar, ambao ni sehemu ya baraza hilo. 
Lakini akasema ina Baraza la Mawaziri la watu 54 ukilinganisha na Marekani, ambayo ni nchi tajiri ya kwanza duniani yenye GDP ya trilioni 14 zaidi ya mara elfu moja ya Tanzania, lakini baraza lake la mawaziri lina watu 15 tu.
 Lyimo alisema pia Japan, ambayo ni nchi ya tatu kwa utajiri duniani yenye GDP ya dola za Marekani trilioni 5, bado ina Baraza la Mawaziri la watu 17 tu, wakati nchi ya Ujerumani, ambayo ni nchi ya nne kwa GDP, ina Baraza la Mawaziri la watu 15 tu.
Alisema suala la kuhamia Dodoma, limekuwapo toka mwaka 1976, ambapo mpaka leo ni miaka 35, sawa na miezi 420, bado serikali haijahamia huko.
CHANZO: NIPASHE