Polisi ya Ugiriki imetumia gesi ya kutoza machozi katika mapambano yanayoendelea hapa na pale dhidi ya vijana wanaorusha mawe mjini Athens, ambako mgomo wa saa 48 unafanyika kupinga kura inayotazamiwa bungeni juu ya hatua kali za kufufua hali mbovu ya Uchumi.
Maelfu ya waandamanaji walikusanyika nje ya bunge la nchi hiyo katika mji mkuu ambako usafiri wa umma umekwama kabisa.
Waziri Mkuu George Papandreou amesisitiza kuwa ni mpango wake tu wa Euro bilioni 28 ndiyo utakaoiwezesha Ugiriki kurejelea hali yake ya kawaida
Endapo mpango huu utakataliwa na bunge, basi Ugiriki itaishiwa na pesa katika kipindi cha majuma machache yajayo.

Maandamano ya jumatatu yalianza kwa amani, lakini yakalipuka na vurumai kuanza hapa na pale.
Baadhi ya waandamanaji walianza kuwarushia polisi mawe na chupa upande mmoja wa medani ya kati mwa mji ijulikanayo kama Syntagma Square, ambapo polisi nao walijibu kwa kufyatua gesi ya kutoza machozi ili kuwadhibiti waandamanaji.
Inaonekana kana kwamba moto ulianzishwa na waandamanaji.
Mgomo huu mkubwa umeathiri huduma za umma, benki zimefunga kazi na hospitali zina wafanyakazi wachache mno.
Viwanja vya ndege vimekuwa vikifungwa kwa saa nyingi, wakati wasimamizi wa kuelekeza ndege wakijiunga na mgomo baina ya saa mbili hadi sita mchana na kumi na mbili jioni hadi saa nne za huko Ugiriki.
.