Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad(Pichani), amesema wakati umefika Zanzibar kunufaika moja kwa moja na misaada kwa ajili ya maendeleo ya sekta ambazo sio za Muungano.
Alitoa ombi hilo jana alipokutana na ujumbe kutoka Shirika la Misaada la Kimataifa la Marekeni (USAID), ofisini kwake Migombani mjini hapa jana..
Maalim Seif alisema kutolewa kwa kasma hiyo moja kwa moja kwa Zanzibar kutaepusha uwezekano mkubwa kwa kuitelekeza miradi ya maendeleo isiyokuwa chini ya sekta za Muungano “kusahauliwa.”
Akitoa mfano alisema sekta ya kilimo sio ya Muungano na inatekelezwa na Serikali ya Mapinduzi kwa kuzingatia sera ya kilimo ya Zanzibar, hivyo sio vibaya kwa nchi na taasisi za misaada za kimataifa kutoa moja kwa moja kwa Zanzibar misaada yao.
“Kuna masuala ya Muungano na yasio ya Muungao, kilimo sio suala la Muungano, Zanzibar ina mambo yake , ni vyema ikapewa kasma yake kuepusha kusahauliwa wakati wa utekelezaji,”, alisema Maalim Seif.
Alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa inaelekeza nguvu zake zaidi katika kilimo cha umwagiliaji na tayari imetenga hekta 8,000 kwa ajili ya kilimo hicho.
Hata hivyo, kati ya hizo, ni hekta 2,000 ndio zimeendelezwa kwa msaada wa serikali ya Korea Kusini.
Kuhusu mradi wa elimu utakaohusisha matumizi ya Teknolojia ya Komputa maskulini (education for 25 th Century), Maalim Seif alisema mradi huo ni muhimu katika karne hii ya 21 ambapo duniani imejikita katika matumizi ya teknoljia ya Habari na Mawasiliano.
Mapema kiongozi wa ujumbe huo wa USAID, Robbert Cunnane, alisema Shirika hilo linalenga kusaidia Zanzibar katika miradi ya kilimo cha umwagiliaji, uzalishaji wa mboga mboga pamoja na huduma za afya.
Alisema mradi wa kilimo utanufaisha zao la mahindi na USAID linakusudia kusaidia eneo hilo.
Aidha Maalim Seif alizungumzia suala la kuimarisha sekta ya elimu, uhifadhi wa mazingira na udhibiti wa maradhi ya malaria, ambapo Mrekani ni mfadhili mkubwa katika ufanikishaji wa mradi wa malaria Visiwani.
CHANZO: NIPASHE
1 Comments