KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, amesema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ndiye Waziri Mkuu pekee anayeishi maisha ya kawaida barani Afrika na gharama zake za maisha ni ndogo kuliko hata za baadhi ya viongozi wa Chadema.

Nape alisema hayo jana akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika viwanja wa sekondari ya Msakila mjini hapa katika ziara yake ya kwanza mkoani Rukwa tangu ateuliwe kushika wadhifa huo.
 
"Sisi sote Pinda tunamfahamu ... napenda kukuhakikishieni, kwamba Pinda ndiye Waziri Mkuu pekee Afrika anayeishi maisha ya kawaida, ni mwungwana kwa kauli na vitendo,” alisema Nape na kuwataka wananchi hao kukataa upotoshaji wa viongozi wa Chadema.

Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alipokuwa Katavi ambako Pinda ni Mbunge, alidai Waziri Mkuu alikuwa anafurahia anasa za cheo chake.


Akiwa katika vijiji vya Majimoto, Mbende na Usevya alikozaliwa Pinda, Dk. Slaa alidai Waziri Mkuu na wasaidizi wake wanatembelea magari ya gharama kubwa wakati wapiga kura wana hali ngumu ya maisha.


Nape alisema Chadema wanamtuhumu Pinda kuishi maisha ya anasa wakati viongozi wa Chadema, akiwamo Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe, ambaye ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, akiishi maisha ya gharama za juu kuliko Waziri Mkuu.


Alidai kuwa Mbowe alipopata nafasi hiyo bungeni, aliilazimisha Serikali impe gari la kifahari aina ya Toyota Land Cruiser V8 ambalo alidai gharama zake ni mara mbili ya gari analotembelea Pinda.


Nape alisema Serikali ya CCM inakusudia kupeleka muswada bungeni unatenganisha siasa na biashara ili wafanyabiashara wabaki kwenye biashara, kwa kuwa wanasiasa kujiingiza katika biashara kunachangia ukwepaji kodi na kuliingizia taifa hasara.


"Wanasiasa kama Mbowe tutawabana, waamue kati ya siasa na biashara, kwani wanachangia kukwepa kodi ambao ni wizi huku wakijifanya wanatetea wananchi.


“Kwa mfano namshangaa sana Mbowe, kwa kuamua kubariki mshahara wa Sh milioni saba anaolipwa Dk. Slaa kuwa eti ni posho!” alishangaa Nape.


Alisema, baraka hizo za Mbowe kwa mwaka zinasababisha Taifa kupata hasara ya Sh. milioni 25 na kwa kuwa watendaji wengine wa Chadema pia wanalipwa posho badala ya mishahara, kwa ujumla wanaliingizia Taifa hasara ya Sh. milioni 487.


Alifafanua kuwa, fedha hizo ambazo ni hasara hiyo inayosababishwa na Chadema kugeuza mshahara kuwa posho ili isilipwe kodi wakati wafanyakazi wengine wote wanatozwa kodi, zingeweza kununua vitabu vya Sayansi 48,000 kwa sekondari nchini na madawati mengi.


Kuhusu tuhuma kuwa alitaka kuhama CCM na kujiunga na CCJ, Nape alisema, kamwe hawezi kukihama chama hicho kwa sababu ni cha waungwana, kwa kuwa kiliasisiwa na waungwana.


Alisema mambo ya CCM ni ya kimungu, ndiyo maana Watanzania wameendelea kukiamini na kukipa ridhaa ya kuongoza nchi kwa amani na utulivu.