Hatimaye Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, amewasilisha rasmi kwa Katibu wa Bunge malalamiko dhidi ya uamuzi wa Spika wa Bunge, Anne Makinda, wa kumkataza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kujibu bungeni swali lake kuhusu mauaji yaliyofanywa na askari wa Jeshi la Polisi dhidi ya wananchi katika maeneo ya Mgodi wa dhahabu wa North Mara, Nyamongo, katika Wilaya ya Tarime, mkoani Mara.
MH: Tundu Lissu mbunge wa Chadema
Kwa mujibu wa waraka wa malalamiko hayo wenye kurasa nne, ambao NIPASHE inayo nakala yake, Spika Makinda alimkataza Pinda kujibu swali hilo kwa hoja kwamba, lilikuwa mahakamani.
Spika Makinda alichukua uamuzi huo wakati wa kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu, bungeni, Juni 26, mwaka huu.
Lissu, ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, aliliambia NIPASHE ofisini kwake mjini Dodoma juzi kuwa aliwasilisha malalamiko hayo kwa Katibu wa Bunge juzi.
Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, alithibitisha jana mjini hapa ofisi yake kupokea waraka wenye maelezo ya malalamiko ya Lissu dhidi ya uamuzi wa Spika Makinda.
Kwa mujibu wa waraka wa malalamiko hayo, hatua hiyo ya Lissu inazingatia kanuni ya 5 (4) ya kanuni za kudumu za Bunge ya mwaka 2007.
Kanuni hiyo inatamka kwamba: “Mbunge yeyote ambaye hataridhika na uamuzi wa Spika anaweza kuwasilisha sababu za kutoridhika kwake kwa Katibu wa Bunge ambaye atawasilisha malalamiko hayo kwa Spika.”
Kwa mujibu wa kanuni ya 5 (5) na (6), baada ya malalamiko hayo kuwasilishwa kwa Katibu wa Bunge, kitakachofuatia ni Spika kuwajibika kuitisha kikao cha Kamati ya Kanuni za Bunge na kulijulisha Bunge kuhusu uamuzi utakaotolewa na kamati hiyo.
Tayari Spika Makinda alikwishaweka bayana msimamo wake kwamba, yuko tayari kuhojiwa na kamati hiyo iwapo ataitwa.
Katika malalamiko yake, Lissu anatoa sababu kuu mbili. Ya kwanza ni kwamba, swali alilomuuliza Waziri Mkuu siku hiyo halikuhusu jambo lolote, ambalo linasubiri uamuzi wa mahakama yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sababu ya pili, anasema kesi namba 210 ya mwaka 2011 inayomhusu yeye pamoja na washtakiwa wengine saba katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime, haina uhusiano wowote na masuala ya Nyamongo.
Lissu anasema katika malalamiko yake kuwa hoja ya kuhusisha kesi yake na masuala ya Nyamongo, iliibuliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, bungeni siku hiyo, wakati haikuwa sahihi.
Pia anasema yeye pamoja na Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Esther Matiko, hawakabiliwi na kesi yoyote ya jinai inayohusu jambo lolote lililotokea mahali popote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vilevile, anasema kesi dhidi yake na wenzake, haina uhusiano na eneo la Nyamongo yalikotokea mauaji Juni 16, mwaka huu na hata siku ya nyuma.
Anasema nakala ya hati ya mashtaka, inaeleza bayana kuwa yeye na wenzake wameshtakiwa kwa makosa matatu.
Makosa hayo ni pamoja na kuingia kijinai katika eneo la kuhifadhia maiti la Hospitali ya Serikali ya Tarime saa 4 usiku, Mei 23, mwaka huu; kufanya mkusanyiko usiokuwa halali katika eneo hilo hilo na kwa muda huo huo.
Kosa lingine waliloshtakiwa anasema ni kumzuia mganga na askari na polisi kutimiza wajibu wao kwa kuwazuia kufanya uchunguzi wa maiti za Emmanuel Magige, Chacha Ngaka Chacha, Chawani Bhoke na Mwikane Marwa.
Anasema mashtaka hayo yalisomwa dhidi yao katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime Mei 24, mwaka huu na kwamba, ndio makosa pekee wanayotuhumiwa nayo mahakamani
Anaiomba Kamati ya Kanuni za Kudumu za Bunge kuchunguza malalamiko hayo na kuamua kwamba, swali alilouliza halikuwa kinyume cha kanuni 64 (1) (c) ya kanuni za Kudumu za Bunge ya mwaka 2007.
Vilevile, anaiomba kamati hiyo ya Bunge kumuelekeza Spika Makinda alijulishe Bunge juu ya uamuzi wa kamati kwa mujibu wa kanuni ya 5 (5) ya kanuni za kudumu za Bunge, 2007.
Kaimu Katibu wa Bunge, Joel, alithibitisha Lissu kuwasilisha malalamiko yake dhidi ya Spika Makinda juzi. Hata hivyo, hakuwa tayari kueleza zaidi.
Katika swali lake kwa Waziri Mkuu bungeni, Lissu alitaka kujua kama ni sera ya serikali ya Tanzania kuruhusu jeshi la polisi kuua wananchi bila kuchukuliwa hatua dhidi yao.
Lissu alisema kuanzia Januari, 2008 hadi wiki mbili zilizopita, jeshi hilo Kanda Maalum ya Tarime, ilikuwa imeua wanakijiji 26 wa eneo la Nyamongo, uliko mgodi huo. hilo liko mahakamani
CHANZO: NIPASHE