Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga, ambao ushiriki wao katika mashindano ya Kombe la Kagame mwaka huu ulikuwa unategemea 'huruma' ya waandaaji.
Wamepangwa kuanza kampeni za kuwania ubingwa wa mashindano hayo kwa kuivaa El Mereikh ya Sudan katika mchezo wa Kundi B utakaofanyika Jumapili kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Wawakilishi wengine wa Bara, Simba, ambao wako kundi A, watafungua dimba Jumamosi kwa kuikaribisha Vital'O ya Burundi kwenye uwanja huo huo kuanzia saa 10:00 jioni wakati saa nane mchana Etincelles ya Rwanda itacheza na Zanzibar Ocean View.
Akitangaza ratiba hiyo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah, alisema kuwa jana walipokea barua kutoka kwa waandaaji wa mashindano hayo, Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ikieleza kwamba imeisamehe Yanga kwa kosa ililofanya la kutotokea uwanjani kucheza mechi ya kusaka mshindi wa tatu dhidi ya mahasimu wao Simba, na kusema kwamba wamelipa faini walivyotakiwa kufanya.
Osiah alisema kwamba mashindano katika hatua ya makundi yatachezwa kwenye vito viwili kimoja kikiwa Dar es Salaam ambacho kitahusisha mechi za Kundi A na B na kingine kikiwa Morogoro ambacho kitakuwa na timu nne zitakazounda Kundi C.
Alizitaja timu zilizoko katika kundi C kuwa ni mabingwa watetezi wa mashindano hayo, APR ya Rwanda, St. George ya Ethiopia, Ulinzi (Kenya) na Ports ya Djibout.
Alisema kuwa timu mbili zitakazoongoza katika kila kundi na nyingine mbili zitakazofuatia zitasonga mbele na kucheza hatua ya robo fainali ambayo itaanza kuchezwa kuanzia Julai 4 wakati fainali ikifanyika Julai 9 jijini Dar es Salaam.
"Mwanza na Tanga walituma maombi ya kutaka kituo kingine kichezwe huko lakini gharama za kupeleka timu huko ambazo ni kati ya Sh. milioni 50 na Sh. milioni 70, zimetufanya tuyapeleke Morogoro ambapo ni karibu kusafirisha timu zitakazosonga mbele," alisema Osiah.
Simba itashuka kucheza mechi yake ya pili kwa kuivaa Zanzibar Ocean View na kumaliza hatua ya makundi kwa kukutana na Etincelles wakati Yanga Jumatano itakutana na Bunamwaya na baadaye Elman.
Ratiba hiyo inaonyesha kwamba Jumapili mkoani Morogoro, APR itaanza kampeni za kutetea ubingwa wake kwa kuivaa Ports na mechi yake ya pili itakuwa ni dhidi ya Ulinzi itakayofanyika Juni 29 na kumaliza hatua hiyo ya makundi kwa kuivaa St. George ambayo mwaka jana walikutana kwenye hatua ya fainali jijini Kigali, Rwanda.
Bingwa wa michuano hiyo atajinyakulia kitita cha Dola za Marekani 30,000, mshindi wa pili Dola 20,000 na wa tatu Dola 10,000, zote zikitolewa na mlezi wa CECAFA, Rais wa Rwanda, Paul Kagame. Mashindano hayo yamedhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).