SHEHE Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Salahe Abdallah (76) ambaye aliwahi kuwa Kaimu Shehe wa Mkoa wa Rukwa, amefariki dunia na kuzikwa jana mjini Mpanda mkoani Rukwa.
Alifariki dunia usiku wa kuamkia jana saa nane usiku katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda alipokuwa amelazwa akitibiwa ugonjwa wa mapafu na kuzikwa katika makaburi ya madukani mjini hapa.
Kaimu Shehe wa Wilaya hiyo, Hussen Ally alithibitisha kufariki kwa Sheikh Abdalah na kusema kuwa katika uhai wake amekuwa na wadhifa huo kuanzia mwaka 1994 -2011 alipofariki dunia.
Wakati huo huo, juzi maelfu ya wakazi wa Mji wa Muheza na wengine kutoka wilaya nyingine
za Mkoa wa Tanga na nje ya mkoa huo, walishiriki maziko ya aliyekuwa Shehe Mkuu wa
Wilaya ya Muheza, Athumani Zuberi bin Jumaa (66).
Shehe Athumani aliyeshikilia wadhifa huo kwa miaka 21, alifariki dunia Ijumaa usiku
kwenye Hospitali Teule ya Wilaya ya Muheza baada ya kulazwa akisumbuliwa na ugonjwa
wa moyo.
Alizikwa juzi saa nane mchana kwenye makaburi ya familia yao kijijini Mamboleo, kilometa
chache kutoka Muheza Mjini, katika maziko yaliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya, Mathew
Nasei.
Mbali na Mkuu wa Wilaya, viongozi wengine waliokuwa miongoni mwa wananchi
waliomzika Shehe huyo ni wenyeviti wa CCM wa Wilaya za Muheza na Mkinga, Peter Jambele
na Shehe Mudhihir, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Wilaya, Abdallah Seif
na Katibu wa Bakwata Mkoa, Mohamed Riyami.
Mufti wa Tanzania, Shehe Mkuu Issa Shaaban bin Simba, aliwakilishwa na Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Bakwata Taifa na Mjumbe wa Baraza la Maulamaa, Shehe Ali Luwuchu
ambaye pia ni Shehe Mkuu wa Wilaya ya Pangani.
|
0 Comments