Mechi ya kwanza ya mashindano ya kimataifa ya kuwania ubingwa wa Kombe la Shirikisho kati ya Simba na timu ya DC Motema Pembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inatarajiwa kuchezwa kuanzia saa 9:30 mchana Jumapili kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu', alisema jana kuwa wameamua mechi hiyo ianze muda huo kwa sababu ndio wanaamini watawamudu wapinzani wao ambao wametoka katika mji wenye baridi.
Kaburu alisema kuwa maamuzi hayo yamefanywa kwa kutokana na ushauri wa benchi la ufundi na kuongeza kwamba maagizo yote ili ushindi uweze kupatikana yanayotolewa na idara hiyo yanatekelezwa.
Alisema pia wanawaomba mashabiki wa timu hiyo na wadau wa soka nchini kujitokeza kuishangilia Simba Jumapili ili waweze kufanya vizuri na hatimaye kusonga mbele kwenye mashindano hayo.
Aliongeza kwamba ushindi mnono katika mechi hiyo ya kwanza utawaweka kwenye nafasi nzuri ya kuwakabili wapinzani wao kwenye mchezo wa marudiano utakaofanyika mjini Kinshasa Juni 19.
Alisema kuwa DC Motema Pembe wanatarajiwa kuwasili nchini kati ya leo na kesho ingawa bado hawajatuma taarifa kwa maandishi kama inavyotakiwa.
Alisema pia tiketi za mchezo huo zitaanza kuuzwa mapema na kukitaja kiingilio cha chini katika mchezo wao ni Sh. 5,000 katika eneo la viti vya rangi ya bluu na kijani wakati kile cha juu kwenye eneo la VIP A ni Sh. 20,000, VIP B na C ni Sh. 10,000 huku eneo la viti vyenye rangi ya machungwa vinavyozunguka uwanja huo ni Sh. 8,000.
Alisema pia kamisaa na waamuzi wa mchezo huo ambao wanatoka Nigeria watawasili nchini leo tayari kwa ajili ya kuanza kusimamia mechi hiyo.
Wakati huo huo, Daktari wa Simba, Cosmas Kapinga, aliliambia gazeti hili jana kuwa kipa, Juma Kaseja, ameshapona maumivu ya taya aliyoyapata wakati timu hiyo ilipovaana na Wydad Casablanca ya Morocco jijini Cairo, Misri hapo Mei 28.
Daktari Kapinga alisema kuwa tayari nyota huyo alishaanza mazoezi ya pamoja na wenzake tangu Jumatatu na endapo kocha mkuu, Moses Basena, ataamua kumpanga hakuna tatizo lolote.
Katika hatua nyingine wachezaji wa timu hiyo waliokuwa kwenye kikosi cha Tanzania, Taifa Stars, walitarajiwa kujiunga na wenzao kwenye mazoezi jana jioni huku Jerry Santo, aliyekuwa katika timu ya Harambee Stars, ndiye ambaye hajarejea nchini.
Mshindi kati ya wawakilishi hao wa Tanzania na DC Motema Pembe itakuwa imefuzu hatua ya nane bora ya mashindano ya Kombe la Shirikisho.
Mwishoni mwa mwezi huu Simba pia itapeperusha bendera ya Tanzania Bara kwenye mashindano ya Kombe la Kagame yatakayofanyika hapa jijini Dar es Salaam baada ya kuhamishwa kutoka Sudan kufuatia vurugu za wenyewe kwa wenyewe.
1 Comments
Rekebisha neno TANZANI,inabidi liwe TANZANIA,ongezea ...A