Viongozi nchini wameaswa kufanya kazi kwa bidii na uadilifu mkubwa ili wananchi wanaowaongoza wawaone na kuwasifia kwa kazi waliyoifanya badala ya kupenda kusifiwa hata kama wanachokifanya siyo kizuri kwa wananchi wanaowaongoza.
Wito huo ulitolewa na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa(Pichani juu), wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya jubilei ya miaka 50 ya uaskofu wa Askofu Mstaafu wa Jimbo la Bukoba, Mhashamu Plasidius Gervas Nkalanga yaliyofanyika katika Abasia ya Hanga Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.
Alisema baadhi ya viongozi wamesahau kuwa kazi ndiyo kipimo cha utu na badala yake wanapenda zaidi kusifiwa na kutukuzwa bila wao kutimiza wajibu wao wa kufanya kazi kwa manufaa ya jamii ambayo wanapaswa kuitumikia pamoja na kumwabudu Mwenyezi Mungu ambaye ndiye muweza wa yote.
Akizungumzia Askofu mstaafu Gervas Nkalanga, Rais mstaafu Mkapa alisema kwa kawaida mema ya mtu huzungumzwa baada ya kifo lakini ni bahati kwa Askofu Nkalanga kuzungumzwa mema yake akiwa hai na anayasikia, jambo ambalo ni faraja kwake kusikia uchapakazi wake na ubunifu wake katika mambo ya kiroho na kimwili kwa jamii aliyoishi nayo kwa kipindi chake cha umri wa miaka 92 mpaka sasa.
Naye Askofu mstaafu wa Jimbo la Bukoba, Mhashamu Gervas Nkalanga, akitoa shukrani kwa maaskofu zaidi ya 20 wa Kanisa Katoliki nchini waliokuwepo katika jubilee hiyo wakiongozwa na Mwadhama Policarp Kardinali Pengo, aliitaka jamii kuvumiliana katika mambo yanayoifanya iwe moja kwa sababu hakuna mtu ambaye hana mapungufu duniani.
Alisema viongozi na jamii kwa ujumla wanapaswa kuishi na kujenga utamaduni wa utii, unyenyekevu, upendo na amani vitu ambavyo vinawezekana ikiwa tu kila mmoja atakumbuka kuwa kuna Mungu aliyemuumba na kumwezesha kufika hapo alipo ingawa watu wengi hukumbuka kusali na kumuomba Mwenyezi Mungu baada ya kuzeeka au kuugua sana lakini yeye aliamua kumtumikia Mungu kwa kuwahudumia wanadamu kimwili na kiroho pia bila ukaidi wowote.
Awali, Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Afrika, Yuda Thadei Rwaichi, alisema taifa linahitaji sala za pekee katika kipindi hiki ili wananchi waione nuru na mwanga walioutarajia kuuona vitu ambavyo vitawezekana ikiwa uadilifu utakuwepo katika kila ngazi ya jamii kuanzia kwa viongozi mpaka kwa wananchi wanaoongozwa.
0 Comments