UMOJA wa Mataifa umeipa heshima Tanzania ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa Utumishi wa Umma unaoanza leo jijini Dar es Salaam.
Tanzania imekuwa ya kwanza katika Afrika kuwa mwenyeji wa mkutano huo utakaofunguliwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na ukitarajiwa kufungwa na Rais Jakaya Kikwete.
Mkutano huo wa siku nne unaushirikisha pia Umoja wa Afrika (AU) na unatarajiwa kuhudhuriwa na wageni 500 kutoka nchi 80 za Afrika, Amerika, Asia na Ulaya.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, utakapofanyika mkutano huo, Mshauri Mwandamizi wa Kanda katika Idara ya Utumishi wa Umma na Utawala (UNDESA), Richard Kerby alisema lengo la mkutano huo ni kuongeza uwajibikaji wa sekta ya Utumishi wa Umma.
Kerby alisema, “Kwa mara ya kwanza maandhimisho haya yanafanyika Afrika na Tanzania inakuwa mwenyeji, hii ni heshima ya pekee kwa kuwa kwa sehemu kubwa, amani, utulivu na uwajibikaji hasa kwa kushirikisha sekta binafsi upo hapa ukilinganisha na nchi nyingine”.
Kwa mujibu wa Kerby, katika mkutano huo ambao kilele chake ni Juni 23 ambayo ni Siku ya Utumishi wa Umma Duniani, tuzo mbalimbali zitatolewa ambapo Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita) ni miongoni mwa watakaopokea tuzo.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sera wa Ofisi ya Utumishi wa Umma nchini, Mathias Kabunduguru alisema maadhimisho hayo yamekuja nchini wakati mwafaka kuelekea miaka 50 ya Uhuru.
Alisema, heshima hiyo inadhihirisha nchi inafanya vizuri na ni sehemu ya kuongeza juhudi katika kuimarisha huduma kwa jamii.
Katika mkutano huo unaofanyika sambamba na maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Mnazi Mmoja, mbali na Kongamano la leo, mada mbalimbali zitatolewa na kujadiliwa kuanzia kesho ikiwemo suala la jinsia, uchumi, nguvu ya utumishi wa umma, kuingiza wananchi katika sekta, nafasi ya sekta binafsi na nyinginezo.

0 Comments