KIKONGWE Mathias Kisokota (94) mkazi wa Namanyere wilayani Nkasi mkoani Rukwa, amefunga ndoa na kikongwe mwenzie, Uria Mwimanzi (80).

Ibada ya ndoa hiyo iliyofungwa jana, iliongozwa na mapadri wawili, Paroko wa Parokia hiyo,

Padri Shilari Katindi na Padri Peter Twamba na kuvuta waumini wengi kufurika katika kanisa hilo kushuhudia wazee hao wakifunga ndoa.

Mzee Kisokota na mzee mwenzake wana watoto kumi, na wajukuu zaidi 50 na walianza

kuishi pamoja miaka 35 iliyopita baada ya kufariki mkewe wa kwanza, Agnes Kasinsila.

Jana asubuhi bibi harusi mtarajiwa alipelekwa saluni kupambwa nywele zake na kuvikwa

shela kabla ya kwenda kanisani.

Katika miaka yote hiyo, Mzee Kasokota ambaye ni Mkatoliki Bibi Uria anayesali Kanisa la

Moravian, walikuwa wakishiriki ibada kama kawaida lakini walikosa baadhi ya huduma za kiroho.

Katika mahubiri yake kanisani hapo, Padri Twamba alisema hiyo ni changamoto kwa vijana

kubadilika kitabia na kutenda matendo mema ya kumpendeza Mwenyezi Mungu hasa wakati
huu ambao Jimbo Katoliki Sumbawanga linajiandaa kusherehekea jubilee ya miaka 125 tangu kuanzishwa kwake.

"Hii ni changamoto kwa vijana kubadilika kitabia na kutenda matendo mema ya kumpendeza

Mungu...ni faraja kwetu katika umri wa wazee hawa wameamua kufunga ndoa,” alisema.

Msemaji wa familia hiyo, Filibert Lumbert alisema wazee hao pamoja na kwamba wameanza

kupoteza baadhi ya kumbukumbu muhimu, lakini walisisitiza kila mara kwamba lazima wafunge ndoa kanisani.

Lengo lao kwa mujibu wa Lumbert, ni ili wapate huduma zote muhimu za kiroho kama

ilivyo kwa Wakristo wengine hususani Wakatoliki.

Huduma ambazo wamekuwa wakizikosa ni pamoja kupokea chakula cha Bwana (Sakramenti Takatifu).


Lumbert alisema, maharusi hao pia waliamini wakiendelea na maisha ya bila ndoa

wanaweza kuzikwa nje ya makaburi ya Wakatoliki.

Baada ya kufunga ndoa, sherehe ya kuwapongeza maharusi ilihamishiwa ukumbini.