Mkurugenzi wa kampuni ya Benchmark Prodiction, Madam Ritha Paulsen akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana wakati wa kutangaza uzinduzi rasmi wa shindano la Bongo Star Search.

Mashindano ya kuibua vipaji vya muziki ya Bongo Star Search 2011 (BSS) yanaanza Jumamosi huku yakiwa na mabadiliko makubwa kwa mwaka huu.
Mashindano hayo yanayofanyika kwa mwaka wa tano mfululizo, kwa mwaka huu yamepewa jina la ‘Bongo Star Search Second Chance 2011’.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Benchmark Production wanaoandaa shindano hilo, Ritha Poulsen, alisema kuwa shindano la mwaka huu litakuwa ni tofauti na mashindano yaliyopita ambapo hakutakuwa na usaili na badala yake watakaochuana ni baadhi ya washiriki wa miaka iliyopita ambao hawakufanikiwa kutwaa ubingwa.

"Shindano la mwaka huu tumeliita 'BSS Second Chance' kwa sababu kwa mwaka huu tunawapa nafasi nyingine na ya pekee washiriki ambao hawakufanya vizuri kuanzia mwaka 2006 mpaka mwaka jana, hii itakuwa nafasi yao kuonyesha vipaji," alisema Ritha.
Aidha, alisema kuwa shindano la mwaka huu litawahusisha washiriki 30 ambao watachujwa na kubaki 14 ambao wataingia katika michuano ya kila wiki kwa ajili ya kumpata mashindi wa mwaka huu.
Alisema kuwa mashindano ya mwaka huu yameboreshwa zaidi kuanzia hatua ya uandaaji mpaka zawadi kwa mshindi.
Aliongeza kuwa shindano hilo litaanzwa kuonyeshwa kwenye runinga kupitia kituo cha ITV kuanzia saa 3 usiku siku za Jumamosi na litaanzwa kuonyeshwa rasmi kuanzia keshokutwa.
Alisema zawadi ya mshindi wa mwaka huu imeboreshwa ambapo itatangazwa baadae.
Kwa upande wake, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro inayodhamini mashindano hayo, George Kavishe, alisema kuwa kampuni ya bia nchini (TBL) kupitia bia hiyo wanaendelea kudhamini mashindano hayo ambapo kwa kushirikiana na waandaaji wameboresha zawadi kwa mshindi.
"TBL kupitia bia yake ya Kilimanjaro tunajivunia kuwa sehemu ya shindano hili na kwa mwaka huu mambo yameboreshwa. Siku si nyingi wananchi watatangaziwa zawadi kwa mshindi wa mwaka huu," alisema Kavishe.
Mashindano hayo yalianzishwa rasmi mwaka 2006 ambapo lengo lake kubwa ni kuibua vipaji vya vijaa katika nyanja ya muziki.
Katika shindano la mwaka jana, Mariam Mohamed, kutoka mkoani Mwanza aliibuka mshindi na kuzawadia Sh. milioni 30.