KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, vijana waliochimba kaburi walizuia maiti isizikwe humo mpaka kwanza walipwe Sh 300,000 taslimu kwa kile walichodai kudhalilishwa na wafiwa kwa kuwaita walalahoi wasio na mbele wala nyuma.

Vijana hao walidai baadhi ya wafiwa pia waliwatusi kwa kudai wanachimba kaburi ili angalau wale chakula cha msibani.(Picha hiyo juu haihusiani na habari hii)


Akielezea mkasa huo kwa waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Chanji A, Salvatory Kazumba alisema siku hiyo tukio, vijana wapatao 60 wakazi wa eneo hilo walishiriki kuchimba kaburi kwa ajili ya maziko ya marehemu Mzee Fortnatus Makungu (69) mkazi wa eneo hilo.


Tukio hilo lilifanyika Juni 20, mwaka huu alasiri katika makaburi ya Katandala mjini hapa. Inasemekana vijana hao wakichimba kaburi hilo taarifa iliwafikia kuwa baadhi ya wafiwa wametoa maneno ya kejeli dhidi yao.


“Vijana hao walighadhabika sana baada ya kuelezwa hayo ndipo nilipolazimika kwenda makaburini na kukutana nao......nilikuta kaburi limeshachimbwa na wameandaa mgomba ili usipofikiwa muafaka, basi watauzika mgomba na kutawanyika, lakini pia hata vifaa vya kuzikia vikiwemo majembe, koleo na sururu walikuwa wamevificha kusikojulikana.


“Wakiwa na mshikamano na msimamo wa pamoja, walidai kuwa hataruhusu mwili uzikwe mle mpaka walipwe Sh 300,000 taslimu ili baada ya maziko waende kula hotelini nami niliwafikishia wafiwa ujumbe huo,” alisema Kazumba.


Baada ya wafiwa kufikishiwa ujumbe huo, kulitokea sintofahamu baadhi wakisema marehemu azikwe nyumbani kwake kwani kuna eneo la kutosha huku wengine wakisisitiza azikwe kwenye kaburi lililokuwa limechimbwa.


Hatimaye kwa mujibu wa Kazumba, jeneza lililokuwa na mwili wa marehemu lilipelekwa makaburini kwa maziko ambapo ibada iliongozwa na Padri Boniface Nyama kutoka Parokia ya Kanisa Katoliki ya Familia Takatifu ya mjini hapa.


Baada ya ibada kusomwa, ndipo ilipofuata hatua ya maziko hapo vijana wale waliochimba kaburi walizuia mpaka walipwe kiasi cha fedha walichotaka cha Sh 300,000 taslimu.


Kwa mujibu wa maelezo ya Kazumba, maziko yalifanyika kwa amani na utulivu mkubwa mara vijana wale walipokubali maziko yafanyike baada ya madai yao kukubaliwa.


“Hata hivyo, baada ya vuta nikuvute vijana hatimaye walikubali walipwe Sh 100,000 ambazo zilichangwa na wafiwa na wakakabidhiwa,” alisema Kazumba.