Aliyekuwa Rais wa Misri Hosni Mubarak ni dhaifu na amegoma kula, kulingana na shirika rasmi la habari nchini humo.
Anatarajiwa kufikishwa mahakamani wiki ijayo, akituhumiwa na makosa ya rushwa na kuamuru kufanyika kwa mauaji ya waandamanaji.
Mkuu wa hospitali ambapo Bw Mubarak ameshikiliwa huko Sahrm al-Sheikh amesema alikuwa mnyonge, amepungua uzito, na hakuwa akila vya kutosha kumweka hai, shirika la MENA limeripoti.
Lakini wakosoaji wamesema ugonjwa wa Bw Mubarak ni kama njama ya kuepuka kufikishwa mahakamani.

Wafuasi wa upinzani wanatia shaka ripoti hiyo. Wanaamini mamlaka husika zinajaribu tu kuzuia kuanza kwa kesi ya Bw Mubarak, inayotarajiwa kufanyika wiki ijayo.
Miongoni mwa ripoti nyingi zilizotolewa kuhusu afya ya Bw Mubarak ya hivi karibuni imesema madaktari wake wataamua katika saa za hivi karibuni, iwapo ulaji wake wa hivi sasa hautoshi kumweka hai.
Mwandishi wa BBC Cairo, Jon Leyne, alisema, sasa hivi kuna ushahidi unaozidi kuibuka kwamba ni mtu anayedhoofika kadri siku zinavyoendelea.
Bw Mubarak alipinduliwa mwezi Februari katika ghasia maarufu zilizosababisha vifo vya zaidi ya watu 840.