Wanadiplomasia wote wa Libya wameambiwa wafungashe virago na kuondoka nchini Uingereza, ikiwa ni jitahada za kumchagiza Kanali Gaddafi kwamba "muda wake wa uongozi umefikia ukingoni", Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza William Hague alisema.
Amesema maafisa wa ubalozi wa Libya wametimuliwa na Baraza la Taifa la Mpito la waasi (NTC) wamealikwa kuingia katika ubalozi huo na kuanza kazi.
Waziri huyo wa mambo ya nje amesema Uingereza sasa inalitambua baraza hilo la NTC kuwa ni "serikali pekee inayoongoza Libya".
Balozi wa Libya nchini Uingereza Omar Jelban alitimuliwa mwezi wa Mei.
Waasi wa Libya na majeshi yanayomuunga mkono Gaddafi bado yanapambana, miezi mitano baada ya harakati dhidi ya utawala wa miaka 42 wa Muammar Gaddafi zilipoanza, huku majeshi ya Nato yakizidi kuimairisha amri ya kutoruhusu ndege kupaa nchi humo, suala ambalo linaungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Katika mkutano wa waandishi wa habari siku ya Jumatano, Bw Hague amesema Baraza la NTC limeonesha namna lilivyo tayari "kuanzisha utawala wa kidemokrasia Libya", tofauti na utawala wa Gaddafi ambapo ukatili wake dhidi ya raia wake umemfanya wamuondoe kuendelea kushika hatamu za uongozi".
Amesema kwa sasa Uingereza itakuwa ikishirikiana na NTC "kwa misingi inayotumika kwa serikali nyingine kote duniani" - na kwa maana hiyo Afisa mkuu wa ubalozi wa Libya aliitwa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza kufahamishwa kwamba wanadiplomasia wote wa utawala wa Gaddafi lazima waondoke nchini.
Inaaminika bado wanadiplomasia wanane wa Libya wapo katika ofisi za ubalozi wao eneo la Knightsbridge.
Bw Hague pia amefahamisha hatua za kupiga tanji mali zenye thamani ya paundi milionia 91 zinazomilikiwa na kampuni ya mafuta na sasa zitakuwa chini ya NTC zitakazowasaidia katika "masuala muhimu nchini" Libya.
Ubalozi wa Uingereza nchini Libya ulisimamisha kazi zake mjini Tripoli tangu mwezi wa Februari.
Wiki hii Bw Hague alishauri Kanali Gaddafi hawajibiki kwenda kuishi uhamishoni iwapo ataondoka madarakani, na kusema kuwa hilo ni suala litakaloamuliwa na wananchi wa Libya".
Alipoulizwa kuhusu taarifa za kutimuliwa wanadiplomaisa wote waliosalia, msemaji wa ubalozi wa Libya ameiambia BBC hajasikia hilo na akaongeza:"kwa sasa hatuna jibu."
0 Comments