MKAZI wa Isalalo wilayani Mbozi mkoani Mbeya, Amina Tulianje (18) ameuawa na mumewe kwa kukatwa shoka kichwani.

Sababu ya kifo hicho ndiyo inayoonekana kushangaza, kwani inadaiwa kuwa mumewe Nemes Muyombe, alifikia hatua hiyo, baada ya kukasirishwa na kitendo cha kumpunja kitoweo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Advocate Nyombi, jana alithibitisha kutokea tukio hilo akisisitiza kuwa chanzo cha ugomvi ni kitoweo.

Ilielezwa kwamba, katika tukio hilo, mume alitumia shoka kumkata mkewe na kukimbia huku akiliacha kichwani kwa mkewe.

Kamanda Nyombi alieleza kuwa, mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi iliyoko Vwawa wakati uchunguzi na juhudi za kumsaka mtuhumiwa vikiendelea.

Katika tukio lingine, Kamanda Nyombi alisema mkazi wa Kijiji cha Igogwe, Rungwe, Alex Hezron (22) amekutwa amekufa huku amekatwa koromeo na kutobolewa macho na kutupwa kwenye Mto Igogwe na watu wasiofahamika.



Tukio hilo lilibainika Juni 21 saa 11 jioni Isaka katika Kata ya Ngunga ambako mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa na majeraha hayo.

Aidha, mkazi wa Chemchemi, Uyole, Mbagale Ndunga (73), alikutwa ameuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni kutokana na imani za kishirikina na watu wasiofahamika. Nyombi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na alisema lilitokea Julai 20 saa 6 mchana Uyole.

Naye Ombeni Msigwa (31) wa Uturo, Mbarali, amepoteza maisha kutokana na kipigo cha mumewe, sababu ikitajwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.

Mume wa marehemu, Siasa Njali (32) ambaye amekamatwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.

Kamanda alisema uchunguzi wa matukio yote unaendelea na watuhumiwa wanatafutwa.

                                          (source Hbari Leo)