MKAZI wa mjini Igunga mkoani Tabora, Paul Samwel (40), amejinyonga hadi kufa baada ya mtoto wake kukaidi amri yake ya kutokunywa pombe za kienyeji wakati wa mchana.

Kifo hicho kimetokea Julai 8, mwaka huu saa 12 asubuhi mjini Igunga baada ya Samwel kugundua binti yake, Milembe Paul kwamba alikuwa amekunywa pombe, hali ambayo alipatwa na hasira na kuchukua hatua ya kujinyonga kwa kamba ya katani.


Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Liberatus Barlow, uchunguzi wa awali unaonesha Samwel alijinyonga kutokana na mtoto huyo kukaidi maagizo yake ya

kutokunywa pombe.(Picha hiyo juu haihusiani na tukio la habari hii).



“Nadhani sababu hizo ndiyo zimepelekea mtu huyo kujinyonga na ninapenda kutoa wito kwa jamii iache kujichukulia sheria mikononi kwani hata kujiua ni kosa la mauaji,” alisema Barlow.


Aliwataka wananchi na hasa wazazi kuacha hasira mara watoto wao wanapowakosea heshima na badala yake wawe na subira kuliko kuchukua maamuzi ya kujinyonga bila kuwa na sababu za msingi.


Kamanda Barlow alisema Jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo na limeshaanza mahojiano na baadhi ya watu.


Wakati huo huo, mkazi wa Kijiji cha Majengo, Kata ya Mbuto, Tarafa ya Simbo wilayani Igunga, amekufa baada ya nyumba yake kuchomwa moto na wananchi wenzake usiku wa Julai 8.


Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa, Liberatus Barow, Mungasani Monduki (38), alifariki ndani ya nyumba yake baada ya wananchi hao kuichoma moto kwa tuhuma kwamba anajihusisha na ujambazi.


Mke wa marehemu alinusurika katika ajali hiyo.