RAIS Jakaya Kikwete ameziambia Sudan na Sudan Kusini kuwa bunduki haiwezi kutoa majawabu ya mvutano kati ya pande hizo ambazo zitatengana na kuwa nchi mbili tofauti Julai 9, mwaka huu, 2011, wakati Sudan Kusini itakapokuwa Taifa Huru.

Kikwete amesema kuwa njia pekee ya kupata majawabu sahihi ya mvutano kati ya pande hizo ni kwao kuendelea kuzungumza na kutafuta suluhisho la amani la matatizo yao

kwa njia ya majadiliano.

Rais Kikwete aliyasema hayo Alhamisi wiki hii wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Sudan, Ali Osman Mohammed Taha wakati wa Mkutano wa 17 wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika katika Kijiji cha kisasa kabisa

cha AU cha Sipopo nje ya mji wa Malabo katika Kisiwa cha Bioko, Equatorial Guinea.

Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete alimwambia kiongozi huyo wa Sudan: “Bunduki haiwezi kuwa jibu kwa sababu hata mkipigana hatimaye mtalazimika kuzungumza. Hivyo, kama mnaweza kuzungumza na kukubaliana bila kupigana basi hilo ni bora sana.”


Kwenye mazungumzo hayo, kiongozi huyo wa Sudan alimwambia Rais Kikwete juu ya hatua

ambazo zimekuwa zinachukuliwa kumaliza mzozo wa kisiasa na kiusalama ambao ulizuka kufuatia tukio la karibuni katika jimbo la mpakani la Abyei ambalo mpaka sasa halitakuwa sehemu ya eneo la Sudan ama Sudan Kusini ifikapo Julai 9 na litabakia eneo linalojitegemea.

Katika mzozo huo, majeshi ya pande zote mbili yalipigana yakasababisha upotevu wa maisha

na mali na kulazimisha mamia ya watu kukimbia eneo la mapigano, hatua ambayo ilizusha wasiwasi kuwa hali hiyo ingeweza kusababisha kuvunjika kwa Makubaliano ya Kuleta Amani katika Sudan.

Katika mazungumzo hayo, Makamu huyo wa Rais wa Sudan amemhakikishia Rais Kikwete

kuwa Sudan itaheshimu makubaliano ya CPA ya kuiwezesha Sudan Kusini kuwa Taifa Huru
ifikapo Julai 9, mwaka huu, 2011.

Kiongozi huyo wa Sudan amesema kuwa matatizo mengi ya mvutano kati ya pande hizo mbili

yamepatiwa majibu, isipokuwa suala la mgawanyo wa mapato ya mafuta.