BUNGE la Tanzania limeanza kupoteza utulivu kwenye mijadala ya hoja mbalimbali, ambapo sasa wabunge wamejenga utamaduni wa kutoa kauli za mitaani bila kuheshimu kiti cha Spika.

Hali hiyo ilijitokeza juzi mchana na ikaendelea usiku kwa wabunge mbalimbali kuzomea, na kutoa kauli za kuudhi, ikiwamo ya Mbunge kuambiwa bungeni si sehemu ya kuvuta bangi.


Juzi usiku baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambayo kabla ya kupita, wabunge 61 walisimama kuashiria kuizuia kabla ya kuridhishwa na majibu ya Serikali, Bunge lilivurugika.



Hali ilichafuka wakati Naibu Spika, Job Ndugai alipokuwa akifafanua kauli ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuwa wapinzani ni wanafiki na kufafanua kuwa alikuwa sahihi.


Baada ya kauli hiyo, wabunge, wengi wao wa kambi ya Upinzani, walisimama wengine wakiomba mwongozo na wengine wakitaka kutoa taarifa, wakati hata Naibu Spika hajakaa.


Wakati wabunge hao wakiwa wamesimama na wengine kuzungumza wakati Ndugai akizungumza jambo ambalo ni kinyume cha kanuni, mmoja wa wabunge mwanamume, aliwasha kipaza sauti chake akasema "Kaa chini Spika hapewi taarifa".


Baada ya kauli hiyo, wengine walianza kufungua vipaza sauti vyao na kusema maneno kama "Toka huko", "Hapa si sehemu ya kuvuta bangi" huku mwanamke mmoja akisema "Mwambie huyooo".


Wakati kauli hizo zinatolewa, Naibu Spika Job Ndugai, alikuwa akizungumza na kuwaonya kuwa Kiti cha Spika kina mamlaka ya kuadhibu na ikibidi hata kumtoa mbunge nje.

Lakini sauti hizo zikaendelea na mmoja wa wabunge alifungua kipaza sauti chake wakati Ndugai akizungumza, akasema zaidi ya mara mbili, "Lakini usipotoshe".
Kutokana na mvurugano huo na kwa kuwa muda wa kuahirisha Bunge ulikuwa umefika, Naibu Spika alisema amewadharau wabunge hao kwanza na lakini ikitokea tena atawaadhibu na kuahirisha Bunge.

Kutokana na hali hiyo, Chama cha Waandishi wa Habari za Bunge (BUPAT), kililazimika kutoa tamko kuelezea masikitiko yake kwa tabia mpya ya baadhi ya wabunge kuwasha vipaza sauti kiholela bila ruksa ya Kiti cha Spika na kutamka maneno yasiyo na ustaarabu kwa utamaduni wa Mtanzania.


"Tumesikitishwa na hali hiyo ambayo kama ikiendelea inaweza kushawishi Watanzania kuamini kuwa nidhamu katika madarasa ya shule za msingi ni juu zaidi kuliko ndani ya ukumbi wa Bunge," tamko hilo lililosainiwa na Mwenyekiti wa Bupat, Godfrey Dilunga.


Wakati huo huo, wabunge wa Upinzani wameelezea kusikitishwa na kauli ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, kwamba wao ni wanafiki wakati walikuwa wakitekeleza Ilani yao ya Uchaguzi.


Akizungumza juzi usiku baada ya kuomba mwongozo wa Spika, Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa (Chadema), alisema Sitta aliwaita wao ni wanafiki kwa kutetea posho na kwamba watafia Upinzani.


"Mnafiki hasa ni nani, aliye kwenye chama kimoja huku akijiandaa kuanzisha chama kingine au anayetekeleza ilani ya chama chake," alihoji Msigwa.


Hata hivyo, Ndugai alifafanua kauli hiyo ya Sitta kuwa alikuwa sahihi na aliwalenga baadhi ya wabunge wa Bunge la tisa ambalo yeye alikuwa Spika.


"Aliuliza, kama kweli wabunge hao leo wanalalamikia posho, warudishe zile (za Bunge la tisa) na kama hawawezi na wanapiga kelele leo basi ni wanafiki," alisema Ndugai.


Hata hivyo jana, Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), aliomba tena Mwongozo wa Spika, na alipopewa nafasi alihoji kauli ya Sitta kwa wapinzani wakati kambi hiyo imetoa Makamu wa Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad.

"Katika vyama vya upinzani tuna viongozi makini akiwemo Profesa Lipumba (Ibrahim) na Maalim Seif, kwa kauli ya jana imetuonesha sisi ni watu hovyo hovyo wakati wengine tuliongoza kambi ya upinzani kwa umakini mkubwa hapa," alisema.
Hata hivyo, Ndugai alimjibu Hamad kuwa anajua kanuni ambazo zimeweka wazi kuwa uamuzi wa Spika ni wa mwisho na kwa kuwa ulishatolewa juzi, haruhusiwi kuhoji.