BONDIA David Haye amepondwa baada ya kulalamika kwamba alichapwa na kupoteza ubingwa wa dunia uzito wa heavy kutokana na kuvunjika kidole cha mguu.
Kutokana na hilo, Haye amepachikwa jina la ‘cry baby’ baada ya kushindwa kudhihirisha ubora wake ulingoni na kuishia malalamiko ya kwamba alivunjika kidole.
Bondia huyo wa England, alipokea kipigo ‘heavy’ kutoka kwa Wladimir Klitschko katika pambano lao lililofanyika wiki chache  zilizopita, akidai kwamba alijiumiza kidole chake cha mguu wa kulia na kumsababisha kushindwa kuonyesha upinzani ulingoni.
Promota wa masumbwi, Frank Warren, alisema: “Asingepigana kama kweli kidole chake kilivunjika. Kwa nini anapenda kulialia tu baada ya pambano? Anakera.


“Wakati ubingwa wako unapowekwa kilingeni, unapaswa kupambana kwa nguvu zote, lakini yeye hakufanya hivyo.
“Kulalamikia vidole na mambo mengine ya aina hayo, ni kauli tu ya kutaka kujitetea na kuwakwaza mashabiki wa mchezo huo.
“Kama kweli aliamua kuingia ulingoni kupambana wakati kidole chake kilikuwa kimevunjika, basi anapaswa kuacha kulalamikia hilo.
“Mashabiki na watu wengine waliocheza kamari hakutambua kwamba anachofanya ni kosa kubwa.”
Haye alipoteza ubingwa wake wa WBA kwa pointi, wakati majaji watatu walipompa ushindi Klitschko, ambaye pia anamiliki mikanda ya ubingwa wa WBO na IBF.
Haye, ambaye pia alilalamikia mchezo mchafu kutoka kwenye kipigo hicho, aliwaomba radhi maelfu ya mashabiki waliosafiri hadi Ujerumani kwenda kumshangilia.
Alisema: “Ni kama walikuwa mvuani kwa usiku wote, walitaka kuwa juu, lakini hawakupata nafasi hiyo. Nawaomba radhi wote – nilicheza kwa jitihada zangu zote, lakini sikuwa bora kama nilivyotaka.”
Baadhi ya mashabiki waliolipa pauni 1,000 kununua tiketi za pambano hilo, walionyesha hasira zao baada ya Haye aliyekuwa akichonga domo kushindwa kuonyesha umwamba ulingoni.
Baada ya kipigo hicho, Haye alijipiga kifua na kudai kwamba ataendelea kupambana na kwamba kwake si jambo la kuunga mkono kung’atuka kwa aibu ya kuchapwa.
Lakini, Warren anadhani Haye anapaswa kutundika glovu zake kuliko kuendelea kuwa na ndoto za kupigana na ndugu wa Klitschko, Vitali, katika pambano la ubingwa wa WBC.