Mchumba wa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Josephine Slaa, ameponea chupu chupu kuuawa na majambazi katika eneo la njia panda ya Suma JKT lililopo Mwenge jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusiana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyella, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 11:57 jioni eneo hilo.
Kamanda Kenyella alisema Josephine alikuwa kwenye gari lake lenye namba T 932 ASR aina ya Harrier akipita katika eneo hilo.
Alisema baada ya kufika eneo hilo, alitokea kijana mmoja na kuvunja kioo cha mbele cha gari lake kwa kutumia nyundo. Kamanda Kenyella alisema baada ya kuvunjwa kioo, gari hilo lilipoteza mwelekeo na kuingia mtaroni.
Alisema hali hiyo ilimpa nafasi kijana huyo kuiba simu mbili, kadi tatu za benki, fedha taslim Sh 50,000, pochi, kamera na nyaraka mbalimbali.
Hata hivyo, Kamanda Kenyella alisema baada ya hapo kijana huyo alitoweka na wenzake kwa kutumia pikipiki.
Alisema Josephine aliokolewa na wananchi waliokuwa karibu na tukio na kutoa taarifa katika kituo cha polisi.
Kwa mujibu wa Kamanda Kenyella, gari la Josephine, lilipigwa risasi mlangoni lakini mwenyewe hakupata madhara yoyote.
"Mhalifu hakuwa peke yake, nadhani alikuwa akishirikiana na wenzake kwani huwezi ukawa unapiga nyundo kioo huku unarusha risasi. Ni lazima alikuwa na wenzake," alifafanua Kamanda Kenyella.
Alisema baada ya Josephine kuokolewa na wasamaria wema hao, alipelekwa katika Hospitali ya Mwananyamala kupatiwa matibabu kutokana na kupata mshtuko.
Hata hivyo, alisema hali ya Josephine inaendelea vizuri na alipatiwa matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Kamanda Kenyella alisema polisi wanaendelea na upelelezi wa tukio hilo ili kuwatia mbaroni waliohusika na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Aidha, alisema biashara ya pikipiki imekuwa ni tishio katika siku za karibuni kutokana na watumiaji wake kujihusisha na vitendo vya uhalifu.
Alisema kuna baadhi ya wahalifu wamekamatwa ambao wanajihusisha na biashara hiyo na wengine bado wanaendelea kusakwa ili wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
CHANZO: NIPASHE
1 Comments