Japan imeilaza Marekani kwa mikwaju ya penalti 3-1 na kuwa nchi ya kwanza kutoka bara Asia kushinda Kombe la Dunia kwa wanawake.
Saki Kumagai ndiye aliyefunga mkwaju wa penalti wa ushindi baada ya mlinda mlango wa Japan, Ayumi Kaihori kuokoa mikwaju mwili ya penalti kati ya mitatu ya wanadada wa Marekani.Marekani watajilaumu wenyewe kwa kushindwa kuweka rekodi ya kunyakua Kombe la dunia kwa mara ya tatu, baada ya kumiliki mchezo kwa kipindi kirefu. Lakini pia wanadada hao wa Marekani walishindwa kutumia vyema nafasi walizopata kufunga mabao hasa kipindi cha kwanza.
Wambach mshambuliaji wa Marekani alikuwa tishio kwa ngome ya Japan na alikaribia kufunga wakati mkwaju wake kugonga mwamba na kutoka nje.
Japan, ambao walikuwa hawajawahi kuishinda Marekani katika michezo 25 waliyokutana siku za nyuma, ambapo walifungwa mara 22, walionekana kuwazidi wapinzani wao katika mashambulio ya kushtukiza. Mbinu hiyo ya kushambulia kwa kushtukiza iliwasaidia sana walipocheza na wenyeji Ujerumani katika hatua ya robo fainali na vile vile walipoitoa Sweden hatua ya nusu fainali, lakini ngome ya Marekani ilikuwa ikikabiliana na wanadada hatari wa Japan, Nahomi Kawasumi na Kozue Ando ambao kwa kiasi fulani walifanikiwa kuwatia mfukoni.
0 Comments