Mwekezaji nchini Tanzania, ambaye ni raia wa Marekanni Igor Kucherenko (42), ameweka rekodi mpya kwa kupanda Mlima Kilimajaro hadi kilele ya Uhuru na kuteremka akitumia muda wa saa 35 tofauti na ilivyo kawaida kwa wengi ambao hutumia muda wa siku sita hadi nane.

Akizungumza na NIPASHE mara baada kushuka kupitia geti la Mweka, Kucherenko alisema alipanda mlima huo mrefu zaidi barani Afrika wenye urefu wa mita 5895 hadi kilele cha Uhuru akiwa na mwenzake Klym Yuriy (26), Julai 2 na kurejea Julai 3, mwaka huu.
Kucherenko, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya madini ya MPG ya jijni Mwanza, alisema siri ya mafanikio yake ni kufanya maamuzi kwamba anaweza.
Katika safari hiyo ya aina yake mpanda milima huyo aliongozana na mwongoza watalii, Elias Daniel Mwaraba.
Kucherenko alifafanua kuwa walianza kupanda mlima huo majira ya saa 1: 26 asubuhi kwenye geti la Umbwe Julai 2 hadi kilele cha Uhuru na walifanikiwa kurejea kesho yake hadi geti ya Mweka, majira ya saa 12 jioni.
“Ulikuwa ni uzoefu wa aina yake na mzuri, na hali ya hewa kwa wastani ilikuwa nzuri pia na hiyo ndiyo ilitufanya tufanikiwe kufika kileleni kwa muda mfupi iwezekanavyo,” alisema na kuongeza, hawakubeba kitu cho chote.
Hata hivyo, alisema kufika kilele cha mlima huo kunahitaji mmoja anayetaka kupata kujizoesha na hali ya hewa kabla ya kupanda, na akasema kuwa Mlima Kilimanjaro ni moja ya mlima mzuri ambao amepata kuuona.
Alisema hii ni mara yake ya tatu kufanikiwa kupanda mlima huo ambapo mara ya kwanza ilikuwa mwaka jana alipotumia siku saba na akarudia tena alipokuwa katika timu ya ‘expedition’ kutoka Marekani Februari mwaka jana na walitumia muda wa siku sita.
Mwongozaji wa watu wanaopanda Mlima Kilimanjaro, Mwalaba alisema tangu aanze kazi hiyo mwaka 2004, Kucherenko ameonyesha tofauti kubwa na ya kuvutia.
“Nimepandisha wengi hadi mlimani, lakini sijapata wageni kama hawa…wamenishangaza sana, ruti waliyopita ni ngumu,” alisema.
Alitaja ruti waliyotumia kuwa ni Umbwe hadi Forest Camp ambayo kwa kawaida hutumia muda wa saa 6 hadi 7, Forest hadi Baraneo Camp muda wa saa 6 hadi 7, Baraneo hadi Arrow Camp muda wa saa 4 hadi 5, Arrow hadi Creator camp muda wa saa 6 hadi 7, Creator hadi Uhuru Peak muda wa saa 1 hadi 1 ½. Alisema wageni hao waliteremka kwa kutumia ruti nyingine ya kutoka Barafu Camp, High Camp, Mweka Camp hadi Mweka Gate.
Mwalaba alisema hakuwa na imani kama wangeweza kupanda mlima huo kwa kutumia muda huo kwa sababu ruti hiyo ni ngumu na yenye miamba na miteremko mikali, na akamshukuru Mungu kwa kufanikiwa.