KOCHA wa timu ya Taifa ya Vijana U-23, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amesema anafuatilia kwa ukaribu uwezo wa Mtanzania anayecheza klabu ya Modema FC ya daraja la pili nchini Italia, George Mtemahanji ili kuangalia uwezekano wa kumtumia kwenye mchezo dhidi ya Shelisheli mwishoni mwa mwezi huu.
Julio alisema jana jijini Dar es Salaam baada ya timu hiyo kumaliza mazoezi yake kuwa amemwita kufanya mazoezi na timu hiyo kwa ajili ya kuona uwezo wake na kumjumuisha kwenye kikosi kinachojiandaa na pambano la kirafiki la kimataifa dhidi ya Shelisheli.

“Tumefanya mazoezi kwa siku mbili katika uwanja wa Karume nimemwona uwezo wake si mbaya sana, lakini bado nahitaji muda wa kumfuatilia zaidi,”alisema Julio.

Naamini atatusaidia kukiongezea nguvu kikosi cha timu yetu katika mashindano mbalimbali tutakayoshiriki kwa siku zijazo,”alisisitiza.Hata hivyo; Mtemahanji alisema amefurahishwa kuitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Vijana kwa ajili ya kujaribiwa.


Naamini nitafuzu kulingana na uwezo wa wachezaji wa kikosi cha timu ya Taifa ya Vijana nilivyowaona kwa siku hizi mbili wakicheza,”alisema Mtemahanji.Alisema nafasi ambazo anazimudu kuzichezea ni kiungo mkabaji (namba 6) na beki wa kulia (namba 2).Kwa Mujibu wa Julio kikosi hicho kina mabadiliko kadhaa ya wachezaji ambapo safari hii pia wamemwongeza Mchezaji George Mtemahanji ambaye anacheza soka la kulipwa nchini Italia kwenye Seria B katika klabu ya Modena FC.
Mtemahanji amepewa nafasi na kocha Julio ili aonyeshe kipaji chake..Wachezaji hao ni Juma Abdul (Mtibwa Sugar), Himid Mao (Azam), Babu Ally (Morani), Shabani Kado (Yanga), Salum Abubakar (Azam), Godfrey Wambura (Simba), Jabir Aziz (Azam), Seif Juma (Ilala), Khamis Mcha (Azam), Shomari Kapombe (Simba), Jackson Wandwi (Azam).

Wengine ni Issa Rashid (Mtibwa Sugar), Thomas Ulimwengu (Hamburg SV Ujerumani), Hussein Javu (Mtibwa Sugar), Mohamed Soud (Toto Africans), Jamal Mnyate (Azam), Awadh Juma (Moro United), Salum Kanoni (Simba), Salum Telela (Yanga), Samuel Ngasa (African Lyon) na George Mtemahanji (Modena FC, Italia)