MATUKIO ya wizi kwa kutumia pikipiki, yamezidi kulitikisa Jiji la Dar es Salaam, baada ya jana, wezi kumpora fedha mtu aliyekuwa anaelekea makao makuu ya Benki ya NMB kwenye makutano ya barabara za Maktaba na Jamhuri.

Siku moja kabla ya tukio hilo, watu wanaosadikiwa kuwa majambazi wakitumia pikipiki na silaha, walipora Sh milioni 13 zinazodaiwa kuwa mali ya kampuni ya simu za mkononi ya Airtel.


Tukio la jana lilithibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile, aliyesema kutokana na kukithiri kwa matukio ya ujambazi wa kutumia pikipiki, utaratibu unafanyika ili kuondoa vituo vya pikipiki za kukodi katikati ya Jiji kwa lengo la kuboresha usalama.



Aidha, Kamanda Shilogile alitoa mwito kwa wananchi kuacha kukaa karibu na maeneo ya benki ili kuepuka madhara yanayosababishwa na matuko ya wizi wa kutumia silaha.


Tukio la jana lililoshuhudiwa na mwandishi wa habari hizi, lilitokea saa nne asubuhi na kusababisha hofu kubwa kwa watu waliokuwa karibu na tukio, hasa baada ya majambazi hao kurushiana risasi za moto na polisi aliyekuwa NMB.


Mashuhuda wa tukio hilo walisema majambazi hao walifika Posta Mpya wakiwa na pikipiki na kuegesha katika kituo cha pikipiki za kukodi karibu na kituo cha mabasi ya abiria.


Ingawa inadaiwa kuwa watu wawili walihusika na tukio hilo, mashuhuda walisema muda mfupi kabla ya tukio hilo, watu wanne walifika eneo hilo wakiwa na pikipiki mbili walizoziegesha na kuangalia kila basi lililokuwa linakuja kusimama kituoni hapo.


Mashuhuda hao walisema baada ya robo saa, waliona watu wawili kati ya wanne wakinyang’anyana mfuko na mwanamume aliyeshuka kwenye basi na kuvuka barabara kuelekea upande wa pili karibu na NMB.


Baada ya mwanamume kung’ang’ania mkoba walitoa silaha, jambo lililosababisha kuuachia na kunyoosha mikono juu, na muda mfupi baada ya kupora, walimfyatulia risasi mlinzi wa benki aliyekuwa anafuatilia tukio hilo. Hata hivyo mlinzi huyo alilala chini na kufyatua risasi angani.


Mlinzi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema alishindwa kuwafyatulia majambazi hao risasi kutokana na tabia ya Watanzania kukimbilia eneo la tukio, ambapo waliwazingira majambazi hao.


Katika mazingira ya kutatanisha, askari wa Jiji anayefahamika kwa jina la Nashon Zephania, alikodisha pikipiki kuwafuatilia majambazi hao, lakini waendesha pikipiki wanaopaki eneo la Posta waligoma kumpakia.


Zephania aliwakimbiza kwa miguu huku akipiga filimbi kuashiria hatari jambo lililosababisha wapita njia kukaa pembeni, kitendo kilichowawezesha majambazi hao kupita haraka na kutokomea kusikojulikana.


Hata hivyo haikuweza kufahamika mara moja ziliporwa shilingi ngapi kwenye mkoba huo.


Hata hivyo habari ambazo hazikuthibitishwa, zilidai kuwa mwanamume huyo alikuwa na zaidi ya Sh milioni 100 ambazo alizipata baada ya kuuza nyumba mbili maeneo ya Mbezi, Dar es Salaam.


Mbali ya matukio hayo, wakazi wengi jijini, hasa wanawake wamekuwa na vilio vya mara kwa mara kutokana na kuporwa mali zao, yakiwamo mabegi na watu wanaotajwa kufanya uporaji huo wakitumia pikipiki.