SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema rasilimali ya nishati ya mafuta na gesi haipaswi kuwa suala la muungano na dhamira ya kuliondoa katika orodha ya muungano ipo pale pale.
Hayo yalisemwa juzi na Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati wa Zanzibar, Ali Juma Shumuhuna wakati akiwasilisha makadirio mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2011/2012 katika Baraza la Wawakilishi, mjini hapa.
“Mheshimiwa Naibu Spika suala la uchimbaji wa mafuta na gesi umepewa kipaumbele cha kwanza.....lakini pia suala la uchumi sio katika mambo ya Muungano hivyo mipango ya kuliondoa katika orodha ya mambo ya Muungano upo pale pale,” alisema Shamuhuna.
Alisema kinachofanyika sasa ni mpango wa utekelezaji wa sera ya nishati ambao umeshaandaliwa na kupelekwa katika ofisi ya ubalozi wa Sweden kwa ajili ya kupata udhamini.
Aidha katika kikao hicho, maofisa watendaji wawili wa kampuni ya Rak Gas Tanzania inayojishughulisha na uchimbaji wa gesi walitambulishwa mbele ya wajumbe wa baraza la wawakilishi wakati bajeti hiyo ikisomwa.
Maofisa hao ni Rud Abbma pamoja na George Sebastian Oging kutoka katika kampuni ya Rak Gas Tanzania ambayo inajishughulisha na kazi za utafutaji na utafiti wa gesi Tanzania.
Sebastian alisema; 'Sisi tumealikwa tu na wizara.....tukihitajika katika kazi za uchimbaji na utafuta wa gesi na mafuta tupo tayari kuja na kufanya kazi hizo,” alisema Sebastian ambaye alikiri kuwepo kwa vikwazo katika kazi za uchimbaji na utafutaji wa mafuta na gesi kwa upande wa Zanzibar kutokana na suala hilo kuwa na utata wa muungano.
Mapema Shamuhuna alisema kwamba SMZ imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kufikisha huduma za umeme na maji safi na salama kwa wananchi wake wa Unguja na Pemba.
Alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa unaonesha kwamba asilimia ya 79.6 ya wananchi wanapata huduma za maji safi na salama katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Aliongeza kuwa, mikakati ya SMZ ni kuona huduma ya umeme zinapatikana kwa wananchi wote Unguja na Pemba ikiwemo katika visiwa vidogo vidogo.
Aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba kazi za utengenezaji wa waya mpya wa baharini imeanza kiwandani huko Japan na kazi hiyo itamalizika Julai mwaka 2012 ambapo pia ulazaji wa waya huo baharini inatarajiwa kufanyika Oktoba 2012.
Aliliomba baraza la wawakilishi kuidhinisha jumla ya Sh 5,026,000,000 kwa kazi za kawaida na jumla ya Sh 4,996,902,000 kwa kazi za maendeleo.
0 Comments