JAMHURI ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikipata hasara nyingi kwa kushindwa kuwatambua watu waishio nchini kutokana na kutokuwa na mfumo thabiti wa utambuzi na usajili wa watu kitaifa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameyasema hayo katika ufunguzi wa semina elekezi kuhusu Utambuzi na Usajili wa Watanzania kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Kilimani mjini Unguja.
Dk. Shein alisema kutokuwepo kwa mfumo wa Utambuzi na Usajili wa Watu kumeiathiri Tanzania kwa kiasi kikubwa katika uchumi, masuala ya jamii na usalama.
Alisema athari hizo zinaweza kuwa kubwa zaidi hasa pale Tanzania inapoingia kwenye soko huria la Afrika Mashariki ambapo kwa upande wa Zanzibar nayo inaguswa na kuhusika na athari hizo.
Akizitaja baadhi ya hasara hizo, Dk. Shein alisema ni wananchi kuendelea kuwa masikini kwa kushindwa kupata mikopo katika benki na taasisi za fedha, hivyo usajili huo utasaidia kujikwamua kiuchumi.
Alisisitiza kuwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imekuwa ikipata matatizo na malalamiko mengi kwa kushindwa kumtambua mwanafunzi yupi anastahili mkopo na kwa kiasi gani pia, urudishaji wa mikopo hii umekuwa mgumu kwa kushindwa kuwapata wadaiwa
mara baada ya kumaliza vyuo na hivyo Serikali kupata hasara.
Athari nyingine ni kuongezeka kwa uhalifu unaofanywa na raia wa kigeni na wafungwa
waliomaliza adhabu zao au kuachiwa huru kwa msamaha wa Rais; Serikali kubeba gharama
kubwa wakati wa upigaji kura na kuwalipa watumishi hewa katika mishahara ya watumishi.
Alisema Serikali imekuwa inapata matatizo na kuingia migogoro na wananchi wakati wa
kuwalipa fidia kutokana na kuchukuliwa ardhi au kubomolewa nyumba zao kwa sababu ya kushindwa kumtambua mmiliki sahihi na anachokimiliki.
Kutokana na hayo, alisema imegunduliwa umuhimu wa kutoa vitambulisho, hivyo utaratibu ambao tayari umeshaundiwa mamlaka na kuipongeza mamlaka hiyo kwa hatua iliyofikia ya kupata mkandarasi wa kutengeneza Vitambulisho vya Taifa.
Dk. Shein alieleza matumaini yake makubwa kwa wajumbe hao kuwa semina hiyo itawaongeza ari ya kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kuhusu umuhimu wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi, katika majimbo na maeneo yao wanayoishi.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkazi vitaendelea kuwepo na kutumika kwa madhumuni yale yale yaliyokusudiwa.

0 Comments