TANZANIA imeombwa kuisaidia Gabon kubuni, kuanzisha na kusimamia mitaala inayofaa kuanzisha ufundishaji wa lugha ya Kiswahili katika shule za nchi hiyo kutokana na uamuzi
wa Serikali ya Gabon kuanza kufundisha lugha hiyo tangu elimu ya msingi.

Aidha, Rais wa Gabon, Ali Bongo Ondimba amemwomba binafsi Rais Jakaya Kikwete kusaidia kumpatia mwalimu binafsi wa kumfundisha lugha ya Kiswahili ikiwa ni jitihada

zake za kuonesha mfano wa kuimarisha ufundishaji wa lugha ya Kiswahili kwa wananchi wake.



Maombi hayo mawili ya Serikali ya Gabon yaliwasilishwa kwa Rais Kikwete wakati wa Mkutano wa 17 wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU) uliomalizika usiku wa Ijumaa, Julai mosi, 2011, kwenye Ukumbi wa Kijiji cha AU cha Sipopo, nje kidogo ya mji mkuu wa Equatorial Guinea wa Malabo, ulioko katika Kisiwani cha Bioko.


Viongozi hao wawili, Rais Kikwete na Rais Ondimba walihudhuria Mkutano huo wa siku mbili na Rais Kikwete amekubali maombi hayo yanayothibitisha utekelezaji wa azma yake ya kueneza lugha ya Kiswahili katika Afrika na duniani pote ambayo aliitangaza tokea mwanzoni mwa Urais wake mwishoni mwa 2005.


Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu jana, Gabon inakuwa nchi ya kwanza katika Afrika kukumbatia na kuamua kufundisha Kiswahili shuleni nje ya nchi za Jumuiya ya Mashariki za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda hata kama lugha ya Kiswahili inazungumzwa na mamilioni ya watu nje ya eneo la Jumuia hiyo ndani na nje ya Afrika.