Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linawashikili watuhumiwa wawili waliohusika na uporaji Sh. milioni 12.5 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Juni 13 mwaka huu na kumuua Juma Bresha, mlinzi aliyekuwa akisindikiza gari lililobeba fedha hizo pamoja na kumjeruhi mfanyakazi wa hospitali hiyo, Sabina Massawe kwa risasi.

Kamanda wa Polisi Kanda hiyo, Suleiman Kova, alisema wamefanikiwa kuwatambua watu hao ambao kwa sasa wanashikiliwa.

Wakati huohuo, Kova amethibitisha kukamatwa kwa risasi 14 za silaha aina ya bastola katika msako mkali wa kupambana na uhalifu jijini uliofanyika Juni 22, mwaka huu.

Alisema majambazi walizitupa zikiwa zimefungwa ndani ya mfuko maeneo ya Mbezi Jogoo.

Aidha, alisema wamekamata magari matatu yaliyokuwa yameporwa na wezi pamoja na watuhumiwa sita.

Kadhalika, alithibitisha kukamatwa kwa noti bandia zenye thamani ya Sh. 510,000 na watuhumiwa wawili waliohusika na tukio hili lililotokea Juni 21 mwaka huu katika maeneo ya Sinza Vatican.