BAADA ya kelele za wabunge na wananchi kuhusu vita dhidi ya dawa za kulevya nchini, Serikali imeamua kuweka hadharani mbinu na majina ya wanaodaiwa kuhusika na biashara hiyo chafu. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi katika kuonesha dhahiri kuchoshwa na kelele hizo, amesema atawapelekea wabunge Kikosikazi kinachoshughulikia biashara hiyo, ili kiweke wazi uhalisia wa mambo.

Kwa matumaini ya wengi, kwa hali ilivyo, ilitarajiwa kuwa Serikali kama inawajua watu hao na ushahidi inao, ingeshawafikisha mahakamani badala ya kuwafanya kuwa mada katika semina elekezi za wabunge na mawaziri.



Wakati wowote kwa mujibu wa Lukuvi, Serikali itawaweka hadharani mbele ya wabunge vigogo hao wakiwamo viongozi wa dini na wafanyabiashara wakubwa, wanaojihusisha na uhalifu huo.


Alieleza nia hiyo alipokuwa akitoa sehemu ya majumuisho ya hotuba ya Makadirio ya Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa mwaka huu wa fedha, bungeni.


“Kwa vile wabunge wengi wamelizungumzia sana suala hili la dawa za kulevya, Serikali imeona sasa ikilete hapa bungeni, Kikosikazi kinachopambana na dawa za kulevya, ili kuendesha semina mbele ya wabunge, muweze kuona ni akina nani wanahusika na biashara hii.


“Yamekuwapo malalamiko, kwamba vigogo wanaohusika na biashara hii ni viongozi wa Serikali, lakini mtaweza kuona wahusika hawa wakiwamo wafanyabiashara wakubwa na viongozi wa dini ambao Rais aliwasema, namna wanavyojihusisha na biashara hii zikiwamo mbinu zao, mtaona kila kitu,” alisema Lukuvi.


Alipoulizwa baadaye kuhusu ufafanuzi wa hatua hiyo kama ilikuwa mwafaka badala ya kuwapeleka mahakamani kama kuna ushahidi, Lukuvi alisema Serikali ina taratibu zake za kushughulikia kesi kama hizo.


Baadhi ya wachambuzi walisema huenda hiyo ikawa ni njia ya Serikali kuanika majina ya wahusika hao wa mihadarati kupitia kwa wabunge ili watakapowaona au kuwatambua waguswe na kupiga kelele zaidi.


Vyanzo vingine vya habari, vilisema jana kuwa kitakachofanyika ni Kikosikazi hicho kuonesha mbinu na ikiwezekana hata mikanda ya video ikiwaonesha vigogo hao na hivyo wabunge kuwajua na kuisaidia Serikali kuchukua hatua.


Lukuvi alisema semina kama hiyo imeshafanyika kwa mawaziri wakati wa semina elekezi mjini hapa hivi karibuni, lakini Serikali imeona umuhimu wa kuendesha semina kama hiyo kwa wabunge ili wajionee hali halisi ilivyo.


Waziri Lukuvi alimtaja Askofu wa Kanisa la Lord’s Chosen Charismatic Revival lenye makao makuu yake Kinondoni Biafra, Dar es Salaam kuwa ni mmoja wa viongozi wa dini waliokamatwa na dawa za kulevya, baada ya kukamatwa na kilo 81 za cocaine eneo la

Kunduchi Mtongani, Dar es Salaam.

Alisema Askofu huyo raia wa Nigeria, anaongoza Kanisa hilo ambalo lina matawi Mwanza, Arusha, Kenya, Afrika Kusini na Uingereza.


Alisema kesi hiyo sasa iko mahakamani.


“Baada ya kumkamata tulipoanza kuwauliza waumini wa Kanisa hilo ni wapi alipo Askofu wao, wote hawakujua lakini baadhi wakisema amesafiri na wengine wakiwa hawana majibu bila kujua kuwa tunamshikilia,” alisema Lukuvi.


Alisema Serikali itaendelea kuwashughulikia na kupambana kwa nguvu zake zote na watu wanaohusika na biashara ya dawa za kulevya nchini bila kujali nafasi zao katika jamii.


Hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete alisema biashara ya dawa za kulevya imeanza kuwavutia hata viongozi wa dini, ambao hata hivyo walionekana kuhamaki wakimpa Rais muda wa saa 48 kutoa ushahidi wa majina, vinginevyo itakuwa aibu kwake.


Hata hivyo, Ikulu ilisisitiza msimamo wake ikisema maaskofu si malaika na baadhi yao wanajihusisha na biashara hiyo.