Juzi, Rostam alitangaza kujiuzulu ubunge na ujumbe wa Halmashauri ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma.
Lowassa alisema ingawa ni haki ya Rostam kujiuzulu katika nyadhifa hizo, lakini hakutegemea kwamba angejiuzulu nafasi ya ubunge.
Alisema alisikitika sana baada ya kuona katika vyombo vya habari jinsi wanachama wa CCM) walipokuwa wakianguka chini baada ya mbunge wao kuwatangazia kuachia nafasi zote za uongozi.
Alipohojiwa kuhusiana na tuhuma zilizoelekezwa kwake wakati wa vikao vya juu vya CCM Aprili, mwaka huu na kutakiwa kujiondoa katika uongozi, Lowassa alisema: “Nitawajibu wakati mwafaka utakapowadia.”
SPIKA: ROSTAM HAJANITAARIFU
Wakati huo huo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, amesema ofisi ya Bunge haijapokea taarifa za Rostam kujiuzulu ubunge.
Alitoa kauli hiyo bungeni jana, baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu ambapo Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Kabwe Zitto, aliomba kupata taarifa ya Bunge juu ya kujiuzulu kwa Rostam na ni lini suala hilo litatangazwa rasmi ili kampeni za uchaguzi mdogo zianze jimboni Igunga.
Zitto aliuliza: “Ni nili utatangaza ili tukachukue jimbo letu?”
Makinda alijibu: “Bado sijapata taarifa rasmi na mimi nimeona kwenye mitandao kama mlivyoona ninyi, hakuniandikia, lakini tutatoa taarifa wakati mwafaka tutakapoletewa taarifa.”
CCM: TUNASUBIRI TAARIFA
Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, alisema Rostam hajawasilisha rasmi barua yake, lakini chama kinaisubiri na kuiwasilisha katika NEC.
MOSHI WAZUNGUMZA
Baadhi ya wakazi wa mji wa Moshi wamekuwa na maoni tofauti juu ya hatua ya Rostam kujivua gamba huku baadhi wakisema ni kukiimarisha chama na wengine ni ukomavu wa kisiasa.
Jaffary Ally, aliyegombea ubunge Jimbo la Moshi mwaka 2010 kupitia CCM, alisema ni hatua njema kabisa kwa afya ya chama kwa kuwa wote wanaotajwa katika suala la ufisadi ambalo linakichafua chama wajiondoe mapema kabla ya kuondolewa.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara na Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, alisema ni uamuzi wa busara kwani amepokea maoni ya wanachama na kuyafanyia kazi.
Naye Katibu wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Basil Lema, alisema:
“Hadi sasa hajakabidhi barua rasmi ya kujivua nyadhifa zote alizokuwa nazo hali ambayo inanipa shaka.” Mwenyekiti wa CCM mkoani Kilimanjaro, Vick Nsilo Swai, alisema uamuzi huo ni wa kikomavu katika siasa na ni kiongozi mtii kutokana na kutii maagizo ya NEC na pia anaelewa kile ambacho viongozi wa ngazi za juu wanachokisema.
Peter Lyimo, mkazi wa Majengo alisema Rostam kama kiongozi amewajibika na kutoa nafasi ili taratibu nyingine zichukuliwe.
MKOA WA MWANZA
Wakazi wa Jiji la Mwanza wametoa maoni tofauti kuhusu hatua ya Rostam huku baadhi wakidai kuwa alichelewa kujiuzulu.
Katibu Mkuu wa Chadema Mkoa wa Mwanza, Wilson Mushumbusi, alisema alitoa uamuzi huo akiwa amechelewa kwani alitakiwa kujiondoa tangu mwaka 2008 wakati wa kashfa ya Richmond.
Mushumbusi alisema Rostam amekuwa akituhumiwa kwa kashfa nyingi, hivyo kama angekuwa na busara uamuzi huo angeuchukua siku nyingi.
Pia, alisema kuwa kujiuzulu kwa Rostam ni mwanzo wa mafanikio ya Chadema kwani Rostam amejiengua kutokana na shinikizo kubwa kutoka kwa wananchi na Chadema juu ya tuhuma za ufisadi.
Alisema hilo halitoshi kwani Serikali sasa inatakiwa kuchukua hatua haraka kumpeleka mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Mwanza, Josephat Ngolangwa, alisema Rostam ameonyesha ukomavu wa kisiasa na maamuzi yake yamekinusuru chama.
Mhadhiri Msaidizi wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano ya Umma wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Sauti), Getrude John, alisema ni uamuzi mzuri kwa maendeleo ya nchi.
Alisema kuwa kutokana na malumbano mengi yaliyokuwepo kuhusu tuhuma mbalimbali kama Richmond na nyingine.
MKOA WA MBEYA
Baadhi ya wakazi wa Jiji la Mbeya wamesema uamuazi wa Rostam utarudisha imani kwa wananchi ambao walikuwa wanakiona kimepoteza mvuto na mwelekeo kwa CCM.
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Shadrack Makombe, alisema uamuzi alioufanya ni mzuri kwani ameonyesha ni jinsi gani amekomaa kisiasa na ni mfano wa kuigwa kwa viongozi wengine ambao wapo ndani ya chama.
Makombe ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu Vijana, alisema kulingana na hatua hiyo inaonyesha dhahiri kuwa CCM inatekeleza suala zima la kujivua gamba kwa viongozi ambao wamekuwa wakinyoshewa vidole na wananchi wakiwemo wanachama wa CCM.
Diwani wa Kata ya Ngonga wilayani Kyela (CCM), Kileo Kamomonga, alisema hatua aliyoichukua Rostam ni ya busara kwani ina lengo la kukirejesha chama kwenye mstari.
Emmanuel Kiketelo Mwamulinge, Mjumbe wa Mkutano wa CCM Taifa, alisema ameitikia agizo la CCM kwamba wale wote ambao siyo wasafi ndani ya chama wajiondoe.
Naye Mwanaharakati na Mwandishi wa habari mkongwe, George Chanda, alisema kujiuzulu kwa Rostam kutaleta ahueni kwa CCM.
Chanda alisema kujiuzulu kwake kutafungua upya njia kwa CCM kuwafuatilia wanachama wake wengine wanaotuhumiwa kuhusika kwa vitendo vya ufisadi ikiwemo wale waliokula fedha za EPA, Richmond, Meremeta, Kagoda ambao wameachwa mitaani bila kuchukuliwa hatua.
Mwenyekiti wa Mtandao wa Wasomi mkoa wa Mbeya, Prince Mwaihojo, alisema hata kama amejiuzulu kwa unyonge, lakini hatua aliyoichukua ni muhimu kwake ili angalau heshima kwake irejee kwani alikuwa amechafuka mno kwa jamii.
CHENGE ATAKIWA KUJIVUA
Baadhi ya wananchi na wana CCM wa Mkoa wa Shinyanga wamemtaka Mbunge wa Jimbo la Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, afuate nyayo hizo. Aidha wananchi hao wameihadharisha serikali na CCM kuwa makini na kumchukulia hatua Chenge kutokana na kuandamwa na tuhuma za ukiukaji maadili.
Baadhi ya wana CCM wamedai kuwa uamuzi wa Rostam hauna budi kuigwa na viongozi na watendaji wengine mafisadi ndani ya CCM na serikali yake kwani ndiyo njia muafaka ya kukinusuru chama hicho ili wananchi wabaki na imani na CCM na serikali yake.
Mmoja wa viongozi wa juu wa CCM wa wilaya ya Shinyanga ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema pamoja na uamuzi mzito wa Rostam, lakini ipo haja kwa serikali na hata chama kuwa makini kwa kufuatilia nyendo za viongozi wengine wenye tuhuma. Mkazi mmoja wa Sima mjini Bariadi, Masunga Mahona, alisema wakati Rostam akichukua uamuzi huo basi na iwe pia busara kwa Chenge naye kufuata nyayo hizo.
UVCCM WAZALENDO
Umoja wa Vijana Wazalendo wa UVCCM wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wameiomba Tume ya Maadili ya viongozi wa Umma kuchunguza kwa makini mali za Rostam aliyejiuzulu juzi kutokana na tuhuma za kifisadi na kumfilisi endapo zitakuwa na taarifa za uongo.
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Umoja huo na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam, Agustino Matefu, jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Alisema tume hiyo ichunguze mali zake zote pamoja na mikataba mbalimbali aliyosaini ili apelekwe mahakamani kwani itakuwa ndiyo dawa kwa viongozi wengine wenye tuhuma.
“Ni vyema tume ikachunguza mali zake kwa umakini na kumfikisha mahakamani,” aliongeza.
Aliongeza kuwa tume pia ichunguze mali za viongozi wanaotoa taarifa za uongo juu ya mali zao wanazomiliki na kuwafikisha mahakamani.
Aidha, Matefu alisema anaiomba serikali iifute Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kwa kutotumia kodi za wananchi vyema.
Alisema anasikitishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah, kudharau tamko walilolitoa Juni 22, mwaka huu linalohusu maombi ya kuchunguza tuhuma mbalimbali za rushwa ya rada, Richmond na Kagoda lililomtaka awafikishe watuhumiwa hao mahakamani.
Alisema wapo tayari kuandamana kuanzia sasa kwani Dk. Hoseah ameonyesha dhahiri kuwadharau kwa kutokufanyia kazi ombi lao walilompa la kuwashughulikia watuhumiwa ndani ya siku 14.
“Sisi tupo tayari kufanya maandamano muda wowote kuanzia sasa pindi tukipata kibali rasmi,” alisema Matefu.
TEC: NI UAMUZI WA BUSARA
Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), limesema uamuzi uliofikiwa na Rostam ni wa busara kwa kuwa unatoa nafasi ya kufanyika uchunguzi zaidi. Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mtendaji wa TEC, Padri Anthony Makunde.
“Mimi naona ni uamuzi mzuri kwa kuwa unatoa fursa kwa taasisi kumchunguza zaidi ili kubaini kama alikuwa na tuhuma zozote,” alisema.
Padri Makunde alisema ni vigumu mtu kuchunguzwa akiwa katika nyadhifa mbalimbali ndani ya taasisi inayomtuhumu hivyo uamuzi wa Rostam anauunga mkono.
Aliongeza kuwa kada huyo wa CCM uamuzi wake haujachelewa kama inavyodaiwa na baadhi ya watu wengi kwa maamuzi yake aliyafanya mwenyewe na kwamba huenda kuna vitu alikuwa anavisubiri.
Imeandikwa na Restuta James na Sharon Sauwa (Dodoma), Salome Kitomari (Moshi) Cosmas Mlekani (Mwanza), Thobias Mwanakatwe (Mbeya), Anceth Nyahore (Shinyanga), Elisante William na Richard Makore (Dar).
CHANZO: NIPASHE
0 Comments