Wasanii mbalimbali wa muziki nchini watawasha moto wa aina yake katika Tamasha la Epiq Nation litakalofanyika siku ya Jmamosi kwenye viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke jijini Dar es Salaam.
Tamasha hilo liloandaliwa kwa pamoja na kampuni ya simu ya mkononi ya Zantel pamoja na kituo cha Redio na Runinga ya EATV ni moja ya mradi mkubwa wenye lengo la kuwapa maisha halisi vijana wa Tanzania.

Akizungumza katika utambulisho wa wanamuziki watakaotumbuiza kwenye tamasha hilo, Mtaalam wa Epiq Nation, Deo Ringia, alisema kwenye mpango huo wameamua kuwapa vijana nafasi ya kuburudika na kuonyesha vipaji vyao mbalimbali kama kuimba, kucheza na kupiga zana za muziki.
Alisema, baada ya kuwarusha ipasavyo wananchi wa Kinondoni kwenye ufukwe wa Coco Beach wiki iliyopita, sasa ni zamu ya Temeke kufurahi pamoja na wanamuziki mbalimbali wanaotamba katika muziki wa kizazi kipya pamoja na taarab.
Epiq Nation ina nia ya kuonyesha maisha halisi ya vijana, tunafahamu vijana wengi wanapenda muziki na mitindo ya mavazi na ndio maana tumeamua kuungana nao,” alisema Ringia.
Aidha, alisema kwenye tamasha hilo hakutakuwa na kiingilio pia kituo cha redio na Runinga ya EATV watakuwa wakitoa matangazo moja kwa moja.
"Ni nafasi nzuri kwa wananchi wa Temeke kufurahi kwa pamoja mbele ya Redio na TV ya East Africa huku wakipata huduma ya simu yenye uhakika," aliongeza kusema.
Baadhi ya washiriki waliotajwa ambao watawasha moto kwa nyimbo zao kali ni pamoja na Juma Nature na kundi lake la TMK Halisi, Bob Junior 'Rais wa Sharobaro', Lulu na mfalme wa taarabu nchini Mzee Yusuph na kundi lake la Jahazi.
Pamoja na hayo, Ringia alisema katika mpango huo wa Epiq Nation, unakwenda sambamaba na utoaji wa zawadi ya simu kwa vijana pamoja na kuwapa ofa maalum ya kutumia bure huduma wa ujumbe mfupi, mtandao pamoja na kunyonya picha 50 kwa siku moja.
Pia kwenye zoezi hilo vijana watapewa wimbo mmoja kwa siku bure na kuwezesha kupiga simu ya Zantel kwenda Zantel kwa senti 10 kwa siku.
CHANZO: NIPASHE