MATUKIO ya ujambazi nchini yamezidi kushika kasi, lakini sita kati ya watu wanaojihusisha na matukio hayo wamejikuta wakikatishwa maisha baada ya kuchakazwa kwa risasi hadi kufa wakati wa mapambano na askari wa jeshi la polisi huko Biharamulo mkoani Kagera.

Hayo yamethibitishwa na Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso aliyesema kwamba, tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia juzi, majira ya saa saba.


Alisema, siku ya tukio wananchi wema walitoa taarifa polisi kuwa, kuna majambazi 6 walikuwa wamesuka mpango wa kufanya utekaji wa magari ya abiria na yale ya mizigo yanayopita katika eneo la pori la Bwanga.



Kutokana na taarifa hizo, askari walivamia pori hilo na kujikuta wakipambana kwa kurushiana risasi na majambazi hao ambao wote walifia katika eneo la mapambano.


Polisi walifanikiwa kupata silaha mbili aina ya SMG na risasi 180 zilizokuwa zinamilikiwa na majambazi hao ambao hata hivyo hawajaweza kufahamika mara moja.


Tukio hilo lilitokea siku moja baada ya mtu anayesadikiwa kuwa ni jambazi, Bhoke Mohere kumpiga risasi na kumuua askari Polisi mwenye namba F. 4268, D/C Pendo aliyekuwa katika utekelezaji wa majukumu ya kikazi kwenye kijiji cha Genkuru wilayani Tarime.


Askari huyo alikwenda kumkamata Mohere nyumbani kwake kwa kosa la unyanganyi wa kutumia silaha na kumiliki silaha isivyo halali. Baada ya mauaji hayo, muuaji huyo alifanikiwa kutoroka.


“Hali hii inaonesha ni jinsi gani askari polisi wanafanya kazi katika mazingira hatarishi, pamoja na kwamba wanakuwa wanatekeleza majukumu yao kwa kufuata matakwa ya sheria, lakini kuna mahali wanakutana na mazingira ya watu wabaya wanaokaidi kutii sheria, hali inayowalazimu polisi nao kutumia nguvu kumdhibiti mhalifu,” amesema Senso.


Kutokana na matukio hayo, ameiomba jamii kuongeza ushirikiano katika kutokomeza vitendo vya uhalifu nchini.


Aidha, amewataka wananchi wanaomiliki silaha bila ya kibali kuendelea kuitikio wito wa kuzisalimisha kwa hiyari, kabla ya kuanza kwa operesheni maalumu baada ya Oktoba 31 mwaka huu.