DIWANI wa Kata ya Idetemya wilayani Geita, Juma Nyembe Machibya (49) wa CCM amepata hasara ya zaidi ya Sh milioni 51 baada ya wananchi wa kijiji cha Nyabulanda kumvamia na kuteketeza kwa moto nyumba zake nne za bati na mali nyingine kufuatia mgogoro wa eneo la kujenga makao makuu ya kata.

Mali nyingine zilizoteketezwa na wananchi hayo ni pamoja na baiskeli tano, mahindi, mpunga, pikipiki, kuku 21, kondoo mmoja na pesa taslimu, sh milioni 1.6.


Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Mugeta Jandwa alisema , tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 4.54 asubuhi katika kijiji cha Nyabulanda wilayani Geita.


Alisema, sababu ya kuteketezwa kwa mali za Diwani huyo ni wananchi wa kijiji cha Idetemya na Nyabulanda kugombea makao makuu ya ya kata yajengwe katika kijiji cha Nyabulanda.


Jandwa alisema, jeshi la polisi linawasaka wananchi waliohusika na tukio hilo ambapo upelelezi ukikamilika watafikishwa kwenye mikono ya sheria kwa hatua zaidi.


Aidha, Jandwa alisema siku hiyo ya tukio majira ya saa 9 mchana wananchi wa kijiji cha Nyabulanda walimjeruhi kwa mawe kichwani Mkuu wa kituo cha polisi Nyangw’ale E. 2534 Koplo Masunga (43) baada ya kutega mawe barabarani.



Mkuu huyo wa kituo alikutwa na zahma hiyo akiwa na Inspekta Barige wakati wakitoka kuwakamata watuhumiwa wa kosa la kutishia kuua kwa maneno katika kijiji hicho ambapo walitega mawe barabarani na waliposimama ndio wananchi walipoanza kumrushia mawe na kumpata kichwani.


Jandwa aliwataja watuhumiwa waliokamatwa kwa tuhuma za kumtishia kumuua Diwani huyo kuwa ni pamoja na Medai Fungame (28), Masumbuko Pius (37) na Stephano Malimi (61).


Hata hivyo alisema hali ya Masunga inaendelea vizuri na kwamba polisi inaendelea na uchunguzi wa tukio ili hatua zaidia za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa waliohusika.