Pichani wavutaji bangi wakiwa ndani ya shamba la miche hiyo.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema kuwa wanaofanya magendo ya mihadarati Afrika sasa wanapitia Afrika Mashariki,
kwa sababu ya vikwazo vingi Asia na Mashariki ya Kati, na hivo kuleta uvunjaji wa sheria na matumizi zaidi ya mihadarati katika eneo hilo la Afrika Mashariki

Inakisiwa kuwa biashara ya mihadarati ilifika dola bilioni 68 dunia nzima, katika mwaka wa 2009.

Ofisi ya Kupambana na Mihadarati na Uhalifu ya Umoja wa Mataifa, inasema ina wasiwasi kuwa Afrika Mashariki imekuwa njia inayotumiwa na wafanya magendo, kwa sababu kanda hiyo haina uwezo wa kupambana na magendo na uraibu wa mihadarati.


Inasema madawa ya kulevya na idadi ya walanguzi waliokamatwa, inaonesha kuwa wafanya magendo hayo, hasa magengi kutoka Afrika Magharibi, wanazidi kusafirisha kasumba kutoka Afghanistan na Pakistan kupitia Afrika Mashariki, kisha kupeleka Ulaya na kwengineko.


Afghanistan ndio mzalishaji mkubwa kabisa wa kasumba, na asilimia 40 hupitishwa Pakistan, kabla ya kuelekezwa kwengineko.

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa inasema katika miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka huu, shehena mbili za kasumba, kila moja zaidi ya kilo mia moja, zimeripotiwa Kenya na Tanzania.

Inaeleza kuwa sababu ya magendo hayo kuzidi ni rushwa, umaskini na uwezo haba wa idara za kuweka sheria.