Mjadala kati ya wanasiasa, kuhusu bajeti, na jinsi ya kuzidisha kiwango cha mkopo wa serikali ya Marekani ungali umekwama.
Ufumbuzi unatakiwa ufikiwe kabla ya Jumaane, ambapo Wizara ya Fedha itaanza kupungukiwa na fedha za kulipia matumizi ya serikali.
Ijumaa usiku, baraza la wawakilishi, ambalo wabunge wake wengi ni kutoka chama cha Republican, lilipitisha mswada kuzidisha kiwango cha mkopo na kupunguza matumizi ya serikali, lakini mswada huo ulikataliwa na baraza la Senate, lenye wajumbe wengi wa chama cha Democrat.
Hali ya uhasama na mashindano imetanda Washington huku Jumaane inakaribia.
Wanasiasa bado wanavutana wakati wanahitaji kupatana ili kuepuka wasi-wasi na pengine matafaruku katika uchumi wa Marekani, ikiwa muafaka haukufikiwa kabla ya tarehe ya mwisho, yaani tarehe mbili Agosti.
Mswada uliopendekezwa na wabunge wa chama cha upinzani cha Republican Ijumaa, katika baraza la wawakilishi, ulizimwa katika baraza la Senate, ambako wajumbe wa chama cha Democrat sasa wanashindana na upinzani, na wanajaribu kusukuma mbele pendekezo lao wenyewe.
Lakini mswada huo piya, uliopendekezwa na kiranja wa chama cha Democrat, Harry Reid, unafanyiwa kazi ili ukubalike kwa wengi.
Vikao kati ya wanasiasa vitaendelea weekendi nzima na huenda makubaliano yakafikiwa dakika ya mwisho, na hatimaye kuwatuliza raia na masoko.
0 Comments