VODACOM Miss Tanzania, Genevieve Mpangala, ametoa msaada wa vitu mbalimbali vikiwemo vyakula kwa wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia wa shule maalumu ya Kilakala iliyopo Manispaa ya Morogoro ikiwa ni moja ya shughuli za kuhudumia watu wenye mahitaji maalumu.
Msaada huo uliotolewa juzi ni pamoja na sukari, mafuta ya kupikia, sabuni, juisi, dawa za meno, miswaki, mafuta ya kupakaa, madaftari, kalamu pipi, mipira ya michezo mbalimbali ambavyo vyote vina thamani ya Sh 300,000.
Akikabidhi msaada huo kwa Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Ayub Nkya, Genevieve alisema ameguswa na maisha ya wanafunzi hao ambao wanahitaji msaada kutoka kwa wadau mbalimbali ili waweze kupata elimu itakayowasaidia katika maisha yao.
Alisema msaada huo utawafanya wananfunzi hao watambue kuwa jamii inawajali na pia utaamsha ari ya kusoma na kujifunza kupitia vitendo na alama ambazo wanazitumia katika maisha yao ya kila siku.
Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa Shule hiyo aliishukuru kamati ya maandalizi ya Miss Tanzania kwa kuratibu ziara na shughuli mbalimbali anazofanya Mrembo huyo, kuwa pamoja na kutoa burudani lakini pia kamati hiyo imekuwa ikisaidia jamii katika nyanja ya elimu, afya na huduma muhimu.
Aidha, mrembo huyo pia alitembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kuwapa pole majeruhi wa ajali ya basi la Hood lililowaka moto eneo la mbuga ya Mikumi Julai 20, mwaka huu.
0 Comments