Aliyekuwa mbunge wa Igunga bwana Rostam Azizi.
SASA ni dhahiri kwamba, uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga upo mbioni kufanyika baada ya ofisi ya Spika wa Bunge kupokea rasmi barua ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Rostam Aziz (CCM).
Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel aliwaambia waandishi wa habari jana ofisini kwake mjini hapa kwamba barua hiyo ya Rostam iliyoandikwa Julai 15 mwaka huu, iliifikia ofisi hiyo Jumanne wiki hii.
Kulingana na Katiba inavyoelekeza kwamba Mbunge atahesabika kuwa si Mbunge tena siku barua ilipopokewa, tangu tarehe Rostam alipotangaza kujiuzulu, alikuwa akihesabiwa kuwa na wadhifa huo kwa maana hata maslahi yake ya ubunge, atalipwa hadi Jumapili wiki iliyopita kabla ya barua kupokewa kesho yake.
Mtendaji huyo wa Bunge alisema taratibu za Mbunge kujiuzulu zinafafanuliwa na Katiba Ibara ya 149 na Sheria ya Uchaguzi, kifungu cha 61(3).
Akizungumzia ibara hiyo ya katiba, alisema mtu yeyote mwenye dhamana ya kazi hususan uwaziri, unaibu waziri na ubunge, anaweza kujiuzulu kwa kutoa taarifa iliyoandikwa yenye saini yake na ataiwasilisha kwa Spika.
“Kwa mujibu wa Ibara ya 149(2) atahesabiwa tangu siku barua ilipopokewa. Kwa mujibu wa barua yake, aliiandika Julai 15 na sisi tukaipokea Julai 19,” alisema kaimu huyo wa katibu wa Bunge.
Joel alisema, baada ya kuipitia barua na kubaini kwamba vifungu vyote vya uamuzi wa kujiuzulu vinajitosheleza, wakamshauri Spika akakubali na wameiandikia rasmi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwamba jimbo la Igunga lipo wazi.
Akijibu maswali ya waandishi waliotaka kufahamu suala zima la mafao, Joel alisema atahesabiwa mafao yake ya miezi saba.
Katika hatua nyingine, gari inayopaswa kutumiwa na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe imeegeshwa karakana huku ofisi ya Bunge ikiwa haina taarifa yoyote ya kukikabidhi rasmi chombo hicho.
“Sisi tulimkabidhi kwa mujibu wa masharti, lakini yeye hajawahi kuandika barua kuwa sharti fulani lina matatizo. Gari halitumiki, hajalikabidhi, lipo kwenye karakana. Gari linatunzwa na Serikali. Akisema analihitaji, sisi tutampa,” alisema Joel.
0 Comments