Chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) cha Hospitali ya Rufaa ya Mnazimoja kitafanyiwa upembuzi yakinifu, chini ya mpago wa kukijenga upya utakaogharamiwa na serikali ya China.
Balozi mdogo wa nchi hiyo, huko Zanzibar, Chen Qiman amesema kazi ya upembuzi yakinifu juu ya hali ya chumba hicho, itafanyika sambamba na kazi nyingine juu ya mfumo wa huduma ya maji na umeme katika hospitali hiyo.
Alitoa ahadi hiyo baada ya serikali yake kutoa msaada kwa Zanzibar wa shilingi milioni 82.5 kwa ajili ya kugharamia mpango wa kujenga uwezo wa watendaji serikalini.
Msaada huo ulikabidhiwa kwa Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar, Omar Yusufu Mzee na Balozi Chen mjini hapa Ijumaa.

Akifafanua juu ya ahadi ya kujenga chumba cha wagonjwa mahututi, Balozi Chen alisema lengo ni kuimarisha huduma kwa wagonjwa na kwamba mpango huo utaambatana na wa mafunzo kwa madaktari.
“Tutakifanyia tathimini kwa lengo la kujua hali ya sasa ya chumba hicho, nia ni kujenga ICU mpya,” alisema Balozi Chen.
Alisema kazi ya awali ya upembuzi yakinifu wa chumba hicho na mfumo wa maji na umeme itatekelezwa na serikali yake kwa ushirikiano na Wizara ya afya na Wizara ya Fedha ya Zanzibar.
Chumba cha wagonjwa mahututi cha Hospitali ya Mnazimoja, hakina vitendea kazi kwa muda wa mwaka moja sasa, baada ya mashine tano zinazowaongoza madktari kujua mwenendo wa afya ya mgonjwa mahututi, kuharibika kabisa.
Mapema mwezi huu, Waziri wa Afya wa Zanzibar, Juma Duni Haji, alitishia kujiuzulu iwapo ahadi ya kuipatia hospitali hiyo vifaa hivyo haitatekelezwa na serikali katika muda wa miezi sita kuanzia mwezi huu.
Hii ilikuwa ni baada ya kubanwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakati wa kupitisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012, wakipinga hatua ya serikali kushindwa kutenga kasma kwa ajili ya manunuzi ya vifaa vya ICU na dawa.
Hata hivyo, wakati Balozi Chen anatoa ahadi juu ya mpango wa kuboresha huduma za Hospitali ya Mnazimoja kwa jumla, Waziri Duni hakuwepo, lakini baadaye alisema amefurahishwa na uamuzi wa serikali ya China kuisaidia Zanzibar katika suala hilo.
Alisema hata katika hatua fulani, baada ya kutishia kujiuzulu serikali alipobanwa na wawakilishi barazani, alipata fursa ya kuonana na maofisa wa ubalozi huo na wakamnong’oneza juu ya mpango wa kujenga upya kitengo hicho.
“Hata uamuzi wangu wa kujiuzulu, waliniuliza nikawaambia, I am serious – sifanyi utani, siogopi kuwa nje ya utumishi wa serikali,” alisema Duni katika mahojiano kwa njia ya simu ya kiganjani akiwa Chukwani.
Akiipongeza serikali ya China baada ya kupokea msaada huo, Waziri Omar alisema utaondoa ukosefu wa mashine za kupima mwenendo wa afya za wagonjwa, kwa sababu ujenzi upya wa chumba hicho, utakuwa ni pamoja na kukiwekea vifaa vya kisasa.
Juu ya msaada wa shilingi milioni 82.5 wa kujenga uwezo wa watendaji serikalini, Waziri Omar alisema fedha hizo zitagharamia mafunzo ya muda mfupi kwa viongozi wa SMZ, wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu, watendaji wa serikali za mitaa na wenyeviti wa kamati za Baraza la Wawakilishi.
Alisema mafunzo hayo yatafanyika nchini China na kwamba washiriki watakwenda katika awamu tatu katika kipindi cha miezi mitatu, kuanzia mwezi ujao, Novemba mwaka huu na Februari mwakani na kwamba jumla ya viongozi 80 watanufaika na mafunzo hayo.