Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wapo hatarini kula samaki wenye sumu baada ya kumpuni moja (jina linahifadhiwa) kudaiwa kuingiza shehena ya samaki hao wanaodhaniwa kuwa na mionzi ya nyuklia.
Habari za uhakika ambazo NIPASHE Jumapili imezipata ni kwamba shehena hiyo ya samaki iliingizwa nchini wiki tatu zilizopita na kampuni hiyo ya jijini kutoka nchini Japan kupitia bandari ya Dar es Salaam.
Watoa habari hizo walisema samaki hao walikuwa wamehifadhiwa kwenye kontena tano zenye uzito wa tani 25 kila moja.
Aidha taarifa hizo zinaeleza samaki hao wametokea mji wa Fukushima ambapo maji ya bahari yaliyozunguka mji huo yameathiriwa na mionzi ya nyuklia iliyotokana na kulipuka kwa vinu vitatu vya mionzi.Japan tayari wamepiga marufuku uuzaji wa samaki wanaovuliwa eneo hilo la bahari.
Vinu hivyo vililipuka baada ya kutokea temekemo kubwa kwenye mji huo na kusababisha mionzi ya nyuklia kusambaa kwenye maji ya bahari.
Imedaiwa kuwa samaki hao kabla ya kufikishwa nchini, walikataliwa nchini humo baada ya Serikali ya Japan kubaini walitoka katika eneo linaloaminika kuwa na mionzi hiyo.
Hata hivyo, baada ya kukataliwa shehena hiyo ilisafirishwa hadi Bandari ya Dar es Salaam na nembo ya kampuni hiyo, ambapo kutokana na kuonekana itakuwa vigumu kukubaliwa kuuzwa sokoni kama itabainika inatoka Japan, kampuni hiyo ilibadilisha nembo na kuonyesha samaki hao wanatoka nchini Indonesia .
Ilibainika makontena hayo yalikaa bandarini hapo kwa wiki tatu wakati uongozi wa Kampuni hiyo ukihangaikia kupata kibali na walifanikiwa kuyatoa makontena hayo Ijumaa iliyopita baada ya kupewa vibali na vyombo husika.
Inadaiwa vibali vya kutolewa kwa makontena hayo vimetolewa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) iliyo chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Idara ya uvuvi iliyo chini ya Wizara ya Mifugo na uvuvi. Viongozi wa TFDA walipotafutwa hawakupatikana kwenye simu zao jana.
Kitu ambacho kinaleta hofu ni baada ya shehena hiyo kudaiwa wakati wowote itaanza kuuzwa kwa wananchi, kitu ambacho kinaweza kuleta madhara kwa binadamu.
Madhara yanayoweza kuwapata walaji wa samaki hao imeelezwa kuwa ni pamoja na kupata saratani, kuharibika kwa mimba pamoja na magonjwa mengine yanayoharibu neva za fahamu.
Aidha, athari endapo mtu atakanyaga mifupa yake kwa bahati mbaya anaweza kudhurika. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda alipopigiwa simu yake ya mkononi kutoa ufafanuzi, alisema kwa upande wake hafahamu tukio hilo.
Alisema ni kweli TFDA ndio wanahusika na utoaji wa vibali kwa bidhaa zote za chakula baada ya kuhakikisha ni salama, lakini kuhusu uingizwaji wa samaki hana taarifa.
“Bwana Mwandishi hilo jambo silijui lakini nashukuru kwa kunipatia taarifa hizo naanza kuzifuatilia sasa hivi,” alisema Dk. Mponda.
Aidha alipopigiwa simu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, David Mathayo hakuweza kupatikana baada ya simu yake kuzimwa.
                                                       NIPASHE JUMAPILI.