Mchezaji wa Azam, Mrisho Ngasa (kushoto) anayefanya majaribio katika timu ya Seattle Sounders ya Marekani akijaribu kumdhibiti Fabio da Silva wa Manchester United wakati timu zao zilipocheza mechi ya kirafiki mjini Washington, Marekani juzi. Man United ilishinda mabao 7-0.

MCHEZAJI Mrisho Ngasa wa Azam juzi usiku alikosakosa kuwafunga mabingwa wa soka wa
England Manchester United walipocheza mechi ya kirafiki na timu ya Seattle Sounders ya
Marekani.

United iko Marekani katika ziara ya maandalizi ya msimu na ilicheza na timu hiyo ambayo Ngassa anafanya majaribio.

Mashabiki wa soka nchini walikuwa na shauku kubwa ya kujua nini atakifanya mwakilishi huyo wa Tanzania katika mechi hiyo ambapo hakufanya ajizi alionesha uwezo mzuri licha ya timu yake kufungwa mabao 7-0 na mabingwa hao walioshika nafasi ya pili kwenye
fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Ngassa aliingia uwanjani kipindi cha pili katika dakika ya 76 na nusura awafunge mabingwa hao katika dakika ya 89 baada ya kupiga shuti kali lililogonga mwamba.



Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye uwanja wa CenturyLink jijini Washington, Manchester ilifunga bao moja katika kipindi cha kwanza na mabao sita yakifungwa katika kipindi cha pili.

Katika mabao hayo, matatu yakiwekwa kwenye kamba na Wayne Rooney aliyeingia kipindi cha pili huku Gabriel Obertan akikamilisha idadi ya mabao hayo dakika ya 89.

Kipindi cha pili kilikuwa cha kasi huku kikiwa na sura mpya ambapo Manchester United walimuingiza Rooney huku Seattle Sounders wakibadili kipa Kasey Keller na kumuingiza
Terry Boss.

Ukiachana na Obertan na Rooney aliyefunga 'hat trick' katika dakika za 52, 69 na 72, wachezaji wengine waliofunga ambao katika mchezo huo ni Michael Owen (dk. 15), Mame Biram Diouf (dk. 49) na Ji-Sung Park (dk. 71).

"Mpaka kipindi cha kwanza kinaisha tulikuwa tumefungwa bao 1-0, wenzetu walicheza vizuri kipindi cha pili na kuweza kutufunga mabao 6, kwani walitumia nafasi zao vizuri huku sisi tukishindwa kumalizia nafasi tulizopata" alisema Sigi Schmid kocha wa Seattle Sounders.

Kocha huyo aliwaomba radhi mashabiki wa timu hiyo waliofurika uwanjani kuiona timu yao ikiboronga katika kipindi cha pili mbele ya mabingwa wenye mataji 11 ya Ligi Kuu ya England huku ikiwa imetwaa mataji matatu ya Ligi ya mabingwa wa Ulaya.

Schmid alikiri kuwa United ni timu nzuri huku akisifia ufundi uliooneshwa na wachezaji hao katika mabao waliyofunga katika mchezo huo huku wakipata kona 6, ingawa alisifia kikosi chake kuwa kilijitahidi licha ya kufanya makosa yaliyosababisha kufungwa idadi hiyo ya
mabao na wao wakiambulia kona 2.

“Nilipanga kuwazawadia wachezaji wangu wote waliopata nafasi ya kucheza katika mchezo huo lakini bahati mbaya wamejikosesha wenyewe,” alisema kocha huyo huku akisikitikia nafasi walizopoteza katika kipindi cha kwanza cha mchezo.

Mashabiki wa timu ya seattle waliofurika uwanjani walihuzunika kuona timu yao ikifungwa idadi kubwa ya mabao lakini kwa upande mwingine walifurahi kuwaona mashetani hao wekundu wenye mashabiki karibu kila pembe ya dunia wakiongozwa na nahodha wao
Rio Ferdinand.